PSG washinda wazomewa kisa Manchester United

Muktasari:

 

  • Kundi la mashabiki wa PSG halikuingia uwanjani hadi baada ya dakika 15 kama sehemu ya kuonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa.

Paris, Ufaransa. Kocha Thomas Tuchel amewasifu wachezaji wake baada ya PSG kuwafunga mahasimu wao Marseille katika mechi yao ya kwanza kwenye uwanja wa nyumbani tangu watolewe katika Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester United.

Goli la utangulizi la Kylian Mbappe lilisawazishwa na Valere Germain, lakini Angel Di Maria alifunga mara mbili na kuisaidia PSG kushinda 3-1 katika mechi hiyo ya mahasimu maarufu kama Le Classique na kupaa kwa tofauti ya pointi 20 kileleni mwa Ligue 1.

Wageni walicheza dakika 28 za mwisho wakiwa 10 baada ya Steve Mandanda kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kushika mpira akiwa nje ya boksi. Di Maria akafunga kwa mpira wa adhabu iliyotinga moja kwa moja wavuni kutokana na kosa hilo la Mandanda.

Kundi la mashabiki wa PSG halikuingia uwanjani hadi baada ya dakika 15 kama sehemu ya kuonyesha kutoridhishwa na timu hiyo kufuatia kutolewa dhidi ya Manchester United mapema mwezi huu.

Tuchel alikataa kuomba radhi kwa kutolewa dhidi ya Manchester United.

“Si suala letu kuomba radhi. Sisi ndiyo tuliofadhaika zaidi. Ilikuwa ni ajali tu,” alisema Tuchel.