PEPIN; Shujaa wa Czech aliyetesa watawala mashabiki wakamuokoa

Muktasari:

Huyu ni Josef Bican (maarufu kwa jina la Pepin, mtu jasiri na mwenye kuvutia) ambaye watu wa nchi hiyo wanasema ni mwanasoka bora kuwahi kulichezea taifa lao.

Siku moja katika mwaka 1964 nikiwa Prague, Jamhuri ya Czech, nikisomea uandishi wa habari niliingia hoteli moja ndogo kando kando ya mto Danube.

Nikiwa ninafurahia chakula ghafla watu walisimama na nilishangaa kwa vile sikujua kilichotokea. Mara alikuja mhudumu na kunitaka nisimame.

Sikubisha kwa vile katika nchi za kikoministi wakati ule jambo dogo lilitosha kukupeleka jela kwa mashitaka ya utovu wa nidhamu kwa utawala.

Nilimuona mzee mmoja amezungukwa na kupigiwa makofi. Kwanza nilifikiri ni kiongozi wa chama cha kikoministi kwa vile viongozi wa chama hicho walikuwa wakiogopwa.

Nilipouliza yule mzee ni nani niliambiwa huyo ndiye “Pepin”, mtu ambaye nilikuwa sijawahi kumuona lakini nilisikia habari zake. Mhudumu alinionyesha ukutani picha yake alipokuwa kijana akiwa anauteremsha mpira kifuani.

Huyu ni Josef Bican (maarufu kwa jina la Pepin, mtu jasiri na mwenye kuvutia) ambaye watu wa nchi hiyo wanasema ni mwanasoka bora kuwahi kulichezea taifa lao.

Siku hizi kila mwaka hufanyika mchezo kumkumbuka mchezaji huyo aliyefariki dunia Desemba 12, 2001 akiwa na miaka 88 na kuacha rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko mchezaji mwingine yoyote wa nchi hiyo. Joseph Bican (Pepin) aliyezaliwa Vienna, Austria, Septemba 25, 1913 ambako ndiko mama yake alikotokea na baba yake alikuwa wa jamii ya watu wa Bohemia, Czech.

Baba yake aliyezechea klabu ya Hertha Vienna ya Austria alifariki akiwa na miaka 30 kutokana na kuumia kwa kupigwa teke tumboni katika mchezo wa kandanda.

Alipofariki baba yake, Pepin alikuwa na miaka minane na miaka minne baadaye alijiunga na timu ya vijana ya Hertha Vienna.

Alipata tabu siku za mwanzo alipotakiwa kucheza na viatu kwa vile alizowea kucheza miguu chini.

Wakati huo mama yake alikuwa mpishi katika hoteli ambayo niliyokuwepo siku ile niliyomuona kwa mara ya kwanza, na ambayo niliambiwa alipenda kuitembelea kumkumbuka mama yake.

Pepin alimsaidia mama yake aliyekuwa na maisha magumu kwa pesa alizotunzwa na watazamaji kila alipofunga goli. Mchezo wake ulivutia vilabu vya Ulaya na kuajiriwa na klabu ya Rapid alipotimiza miaka 18, huku mshahara wake ukiongezwa baada ya kila mezi mitatu alipokuwa na klabu hiyo kwa miaka minne.

Chenga zake za maudhi na hasa kwa kuwafuata wapinzani badala ya kuwakimbia, huku akitabasamu ziliwakasirisha walinzi wa timu alizocheza nazo, lakini aliwafurahisha watazamaji.

Alikuwa bingwa wa kukwepa mikwara na siku moja alipigwa teke la tumbo kama lile lililosababisha kifo cha baba yake. Mama yake, Ludmilla, aliyekuwa akiangalia mchezo ule aliingia uwanjani na mwamvuli na kumtwanga kichwani aliyempiga teke mwanawe.

“ Mulimuua mume wangu mpirani na sasa mnataka kutoa roho ya mwananangu,” alipiga kelele huku akilia.

Moja ya sifa za Pepin aliyewahi kutengenezewa stempu za nchi hiyo, jambo lililokuwa siyo la kawaida kwa vile waliostahiki heshima hiyo walikuwa vongozi wa kikomunisti peke yao, ni namna alivyokimbia kwa kasi na mpira.

Alisukuma makombora makali kwa miguu yote miwili na kupiga vichwa hata mpira uliokuwa juu kidogo tu ya magoti. Siku moja timu yake ilipopata penalti na ikiwa inaongoza 4-0 Pepi alifanya kituko kilichobaki kuwa sehemu ya maisha yake na husimuliwa mara kwa mara.

Kabla ya kupiga mpira alikwenda pembezoni mwa uwanja na kumuomba mama mmoja amuazime kitambaa alichojifunika kichwa, ambacho Pepin alitumia kujifunika uso ili asione.

Baadaye alipiga penalti safi na kufunga bao ambalo watu wa Czech wanalieleza kama goli la kihistoria na magazeti ya nchi hiyo yaliita bao lililofungwa na kipofu.

Pepin aliichezea Austria fainali za Kombe la Dunia za 1934 zilizofanyika Italia na miaka mitatu baadaye alihamia Czechoslovakia na kuchukua uraia.

Aliichezea Slavia Prague na kuwa mfungaji bora wa ligi kwa misimu 12 mfululizo. Baada ya kumalizika Vita Kuu ya Pili ya Dunia 1945, alisakwa na vilabu vya Ulaya, lakini alibaki Prague kwa vile hakutaka kuwa mbali na mama yake.

Alipoambiwa angepewa nyumba kubwa ili aishi na mama yake alijibu: “Je pia mtalihamisha kaburi la baba?” Wakomunisti walipochukua uongozi wa nchi 1948, Pepin alikataa kujiunga na chama cha kama alivyokataa kujiunga na Chama cha Manazi cha Austria kabla ya vita.

Msimamo wake ulimtia matatani 1953 alipokataa kushiriki maandamano ya Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi. Viongozi wa kikomunisti walimuweka gerezani, lakini habari zilipoenea kila pembe vijana walizunguka mitaani na mashambani na kuimba, “Aishi maisha marefu Pepin. Laana kwa watawala.”

Hali ilikuwa tete na watawala walipoona wangeendelea kumuweka gerezani nchi isingetawalika walimuachia. Siku moja maofisa wa usalama wa taifa walikwenda nyumbani kwake na kumwambia alitakiwa Prague kupewa zawadi.

Lakini alipopanda treni wafanyakazi wa treni na abiria waliowafahamu maofisa wa usalama waliofuatana naye walimzuia asisafiri na kwenda kumficha.

Ghasia ziliibuka na safari za treni zilisimama siku kadhaa kutokana na mgomo baridi wa wafanyakazi kupinga njama za wakomunisti za kumdhibiti kipenzi chao, Pepin.

Hatimaye alipoona maisha yake yako hatarini alijiunga na klabu ya chama cha kikomunisti, Dynamo Prague na kuicheza hadi alipostaafu akiwa na miaka 42.

Alipostaafu wakomunisti hawakumjali, lakini watu wengi waliopenda mchezo wake walimsaidia pesa za chakula na matumizi. Baada ya kufanyika mageuzi yaliyosambaratisha utawala wa kikomunisti 1968 klabu ya Tingeren ya Ubelgiji ilimuajiri kama kocha .

Hakuna takwimu sahihi za mabao aliyofunga, lakini inakisiwa yalikaribia 1,000 na kati yao 643 katika ligi za Austria na Czechoslovakia.

Alikuwa mfungaji bora wa Ulaya kwa misimu mitano mfululizo na kila alipopewa zawadi aliomba akabidhiwa mama yake kwa niaba yake.

Pepin alitumia miezi ya mwisho ya maisha yake hospitali akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kwa wastani watu zaidi ya 50 walimtembelea kila siku na kumpa zawadi.

Hivi hivi leo leo sanamu za heshima za mchango wake katika soka zimejengwa katika nci za Austria, Jamhuri ya Czech na ile ya Slovakia.