PATAMU : Hii Vita haina mwenyewe

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastraika ambao wanatunishiana misuli katika ufungaji mabao na mbio zao za kuwania kiatu cha mfungaji bora kinachoshikiliwa na Emmanuel Okwi wa Simba, aliyefunga mabao 20 msimu uliopita.

ACHANA na vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara inayozidi kupambana moto huku, Yanga, Azam na Simba wakitunishiana misuli, utamu wa ligi hiyo buana upo kwenye ufungaji mabao.

Kuna vita kubwa ya wachana nyavu wa Ligi Kuu Bara kwa sasa, japo kasi hairidhishi kulingana na uwiano wa mechi zilizochezwa na idadi ya mabao yaliyowekwa kimiani hasa kwa vinara wanaofukuzana kileleni.

Kwa taarifa yako tu, mpaka sasa zimeshachezwa jumla ya 153 na mabao 280 yakiwa yameshatupiwa kambani, huku nyota wa kigeni 19 wameshafunga jumla ya mabao 60 na huku mabao mengine sita yakiwekwa kimiani na wachezaji waliojifunga wenyewe katika harakati za kuokoa mipira kwenye mechi za Ligi Kuu ya 2018-2019.

Huko kwa sasa ni ubabe ubabe ndilo kauli pekee inayoweza kutumika kwa mastraika wa timu za ligi hiyo, kwani kumekuwa na ushindani mkubwa.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastraika ambao wanatunishiana misuli katika ufungaji mabao na mbio zao za kuwania kiatu cha mfungaji bora kinachoshikiliwa na Emmanuel Okwi wa Simba, aliyefunga mabao 20 msimu uliopita.

ELIUD AMBOKILE-MBEYA CITY

Chipukizi huyu kutoka Mbeya City, Eliud Ambokile ndiye kinara wa mabao kwa sasa akiwa na mabao tisa, akishindana na mastaa wenye mvuto mkubwa kwa jamii ya soka ndani na nje ya nchi.

Ambokile amekuwa akipambana kuhakikisha anaendelea kushikilia rekodi hiyo, tangu alipoipokea kutoka kwa straika wa Simba, Meddie Kagere aliyeongoza akiwa na mabao manne.

Uwezo wake wa kufunga ndio uliwatikisa matajiri wa Simba na Yanga kutaka kumsajili, pia anahitajika na Baroka FC ya Afrika Kusini.

HERITIER MAKAMBO-YANGA

Alianza kwa kasi ndogo lakini kadri siku zinavyoendelea Makambo, amekuwa akiongeza bidii ya kuzifumania nyavu za wapinzani wake, katika mechi 15 walizocheza Yanga amefanikiwa kufunga mabao manane kati ya 29 ya timu yake.

Kasi ya Makambo inampa changamoto Ambokile, pia inaongeza ushindani kwa Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wa Simba.

EMMANUEL OKWI-SIMBA

Okwi ndiye mtetezi wa kiatu cha dhahabu kwani msimu uliopita alifunika mbaya kwa mabao mabao 20, yaliyoisaidia timu yake kubeba ubingwa kwa msimu wa kwanza tangu miaka tano iliyopita.

Msimu huu bado moto wake ni ule ule akiwa amefanikiwa kuzitikisa nyavu za wapinzani wake mara saba, huku akiwa na hat-trick moja aliyofunga dhidi ya Ruvu Shooting.

Okwi atatakiwa kupambana zaidi kuhakikisha anaifikia rekodi yake ya msimu uliopita, lakini pia kuivunja itategemeana na kasi yake ya kuzifumania nyavu, yupo kwenye vita ya ushindani na Kagere na Makambo.

MEDDIE KAGERE-SIMBA

Tangu ajiunge na Simba msimu huu, Kagere amekuwa mpambanaji wa kuzifumania nyavu, tofauti na mwonekano wake wa umri kuwa mkubwa, anamiliki mabao saba, lakini bado anaonekana ana nafasi kubwa ya kufunga, kwanza anacheza kikosi cha kwanza cha kocha Patrick Aussems.

Kagere amekuwa akipambana kwenye mechi ngumu na nyepesi ambazo Simba inakuwa inapata mabao bila kutoa jasho jingi, Kagere atatakiwa kuongeza nguvu zaidi ili kuweza kukipata kiatu cha dhahabu.

SAID DILUNGA- RUVU SHOOTING

Straika wa Ruvu Shooting ya msemaji machachari, Masau Bwire amefunga mabao sawa na mastaa wa Simba, Kagere na Okwi, akiendeleza kasi yake ni dhahiri kutakuwa na ushindani wa hali ya juu kwenye nafasi ya kuwania kiatu cha dhahabu kwa msimu huu.

Dilunga amekuwa kwenye kiwango cha hali ya juu msimu huu kinachomfanya aingie kwenye ushindani wa mastraika wenye mabao mengi.

RAMADHAN KAPERA-KAGERA

Mshambuliaji huyo amekuja kwa kasi, akiwashtua washambuliaji wakongwe kwa namna anavyoibeba kwa sasa Kagera Sugar.

Kapera anakuja kasi kushindana na mastraika wenye mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara, huku akiwa kinara katika timu yake ya Kagera Sugar, akimiliki mabao sita na kama akiendelea na moto wake huenda mambo mbele yakabadilika zaidi.