Ozil achafua hewa tena na demu wake huko Ujerumani

Muktasari:

Ozil ana asili ya Uturuki na alishutumiwa kufanya kampeni za chinichini kumsaidia rais huyo kuchaguliwa tena, licha ya yeye mwenyewe kusisitiza kwamba mazungumzo yake aliyofanya na rais huyo yalikuwa yakuhusu mpira tu.

ISTANBUL, UTURUKI. MESUT Ozil amewachefua tena Wajerumani baada ya kumwaalika kiongozi mkuu wa kisiasa wa Uturuki, Recep Erdogan kwenye harusi yake na mrembo matata wa Kituruki, Amine Gulse.

Ozil mara yake ya mwisho alipokutana na rais huyo wa Uturuki kulizua maneno mengi kwenye mitandano ya kijamii, akishambuliwa hadi kiasi cha kumfanya atangaze kustaafu soka la kimataifa.

Supastaa huyo wa Arsenal amekuwa na imani kwamba alitengwa na chama cha soka cha Ujerumani wakishindwa kumtetea kutokana na mashambulizi ya maneno yaliyokuwa yakielekezwa kwake kisa tu kupiga picha na Erdogan mwaka jana.

Ozil ana asili ya Uturuki na alishutumiwa kufanya kampeni za chinichini kumsaidia rais huyo kuchaguliwa tena, licha ya yeye mwenyewe kusisitiza kwamba mazungumzo yake aliyofanya na rais huyo yalikuwa yakuhusu mpira tu.

Baada ya picha yake aliyopiga na Erdogan kuibuka, kiungo huyo alikuwa akizomewa na mashabiki wa Ujerumani kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, ambapo timu hiyo iliyokuwa mabingwa watetezi walishindwa kutamba na kutupwa nje kwenye hatua ya makundi tu.

Mwezi uliofuatia baada ya kumalizika kwa fainali hizo, Ozil alifuta ukimya na kutangaza kustaafu soka la kimataifa huku akimtuhumu rais wa chama cha soka cha Ujerumani (DFB), Reinhard Grindel kwa ubaguzi.

Grindel alitaka kiungo huyo funsi wa mpira aondoshwe kwenye kikosi cha Ujerumani kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2018 hazijaanza kwa sababu tu ya picha yake aliyopiga na Rais wa Uturuki, picha ambayo pia iliwahusisha kiungo wa Manchester City, Ilkay Gundogan na staa wa Everton, Cenk Tosun.

Bosi huyo wa FA ya Ujerumani hadharani alimtuhumu Ozil kuwa ndio chanzo cha timu yao kuboronga kwenye fainali za Kombe la Dunia, jambo lililomfanya staa huyo wa Washika Bunduki kudaiwa Grindel alikuwa akimsakama tu kwa chuki.

Ozil baadaye alisema alikuwa akisakamwa pia na wanasiasa wa Kijerumani na haikushia hapo, familia yake ilikuwa ikipokea barua na simu za vitisho kutokana na jambo hilo tu. Kutokana na hilo, Ozil aliibuka na kutuma ujumbe wake kwenye mtandao wake wa kijamii, alisema: “Siwezi kuendelea tena kufanywa mbuzi wa kafara kwa mtu mwingine aliyeshindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.

“Machoni mwa Grindel na washirika wake, mimi nakuwa Mjerumani pale tu timu inaposhinda, lakini nakuwa mhamiaji timu ikipoteza.

“Licha ya kulipa kodi Ujerumani, kuchangia vifaa mbalimbali vya shule, kushinda Kombe la Dunia 2014 nikiwa na Ujerumani, bado haitoshi kukubalika kwenye jamii na badala yake nachukuliwa tofauti.

“Kuna vigezo maalumu vya kuwa Mjerumani halisi ambavyo mimi sina?

Marafiki zangu, Lukas Podolski na Miroslav Klose hawaonekani Wajerumani-Wapolandi, hivyo kwanini mimi nionekane Mjerumani-Mturuki? Kwa sababu ni Uturuki? Au kwa sababu ni Muislamu?”

Ozil na mchumba wake, ambaye pia ni Mturuki, amekuwa akitembelea mara kwa mara huko Uturuki na jambo hilo limewaweka karibu sana na Erdogan.

Erdogan ambaye pia alikuwa mwanasoka, amekuwa akidaiwa na wapinzani wake kwa matumizi mabaya ya serikali pamoja na rushwa kwa mujibu wa CNN.

Staa Ozil hivi karibuni alifanya kitendo ambacho kimefichua wazi uhusiano wake mbovu na wakali wawili Mats Hummels na Thomas Muller baada ya kuamua kumpongeza Jerome Boateng peke yake kwa kustaafu soka la kimataifa wakati wakali hao wote watatu walitangaza kustaafu kwa wakati mmoja.

Kitendo cha kuwachunia mastaa wenzake hao kumefungua ukweli kwamba kumekuwa na hali isiyokuwa nzuri baina ya wachezaji hao hasa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018. Wachezaji hao kwa pamoja walikuwa kwenye ushirikiano mzuri wakati Ujerumani ilibeba ubingwa wa dunia kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazil baada ya kuwa na kizazi chenye ubora wa hali ya juu kwa kuwatoa mastaa wengi wakati huo.