Ozil, Romero watemwa Ulaya

London, England. Kipa Sergio Romero, Phil Jones na Marcos Rojo wameachwa katika orodha ya wachezaji wa Manchester United watakaoiwakilisha timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alitoa orodha yake jana ikitoa mshangao kwa wachezaji hao, ambao wameshindwa kumshawishi kocha huyo kuwajumuisha kikosini.

Nyota hao wa Old Trafford hawakuwa na nafasi katika kikosi cha watu 25 kwa ajili ya mashindano hayo, wakiacha nafasi kwa nyota wapya, Edinson Cavani, Facundo Pellistri na Alex Telles.

Mashetani Wekundu wataanza mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain, ambao ni mchezo wa Oktoba 20.

Mchezaji mwingine aliyenunuliwa na Man United msimu huu, Donny van de Beek amejumuishwa kikosini pamoja na wenzake wengine wapya.

Wakati wachezaji waliokuzwa na klabu hiyo, Mason Greenwood, Teden Mengi na Brandon Williams wakiwamo katika orodha B, ambao wanaweza kuongezwa.

Orodhya ya A na B imeonekana kuwachanganya baadhi ya mashabiki, wakati Chelsea ikitoa taarifa ya kufafanua uamuzi wao.

Wakati hali ikiwa hivyo Man United, mchezaji anayelipwa fedha ndefu wa Arsenal, Mesut Ozil naye ameachwa katika kikosi cha miamba hiyo kitakachoshiriki mashindano ya Ligi ya Europa, licha ya kuamua kulipa mshahara wa mshereheshaji wao, Gunnersaurus.

Akilipwa kiasi cha Pauni 350,000 kwa wiki, raia huyo wa Ujerumani, Ozil naye amekumbwa na panga hilo kutokana na kuachwa katika orodha ya watu 25.

Hiyo ina maana kuwa Arsenal angeweza kucheza mchezo wake wa mwisho akiwa na klabu hiyo licha ya kubakiza miezi nane katika mkataba wake wa sasa.