Orkeeswa kidedea michezo ya shule

Muktasari:


Mashindano hayo hufanyika kila mwaka yakizihusisha shule za kimataifa kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Arusha. Shule ya kimataifa ya Orkeeswa imeibuka bingwa wa jumla wa mashindano ya michezo kwa shule za kimataifa nchini mwaka huu yaliyofanyika jijini Arusha juzi Jumapili.

Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha jumla ya shule 12, Orkeeswa ilishinda jumla ya vikombe 14 na medali sita (6) za dhahabu katika michezo nane tofauti ambayo ni soka, mpira wa pete, riadha, raga, mpira wa kikapu, kuogelea, wavu na kurusha tufe.

Vikombe hivyo 14 ambavyo Orkeeswa imetwaa vimetokana na ushindi katika michezo saba waliyoibuka mabingwa kama timu na medali hizo sita zimetokana na ushindi wa mchezaji mmoja katika mchezo wa riadha kwa mbio za Kilomita sita (6) na kilomita nne (4).

Meneja maendeleo wa shule ya Orkeesa, Tunu Makamula alisema mafanikio hayo yametokana na maandalizi waliyoyafanya kwa muda mrefu.

"Wanafunzi wetu wamekuwa wakijiandaa ipasavyo kwa ajili ya mashindano haya. Kutokana na ushirikiano na juhudi zao pamoja na  makocha wao leo tumeona zikilipa na vijana wetu kushinda makombe," alisema Makamula.

Mbali na Orkeesa, shule nyingine zilizoshiriki ni HOPAC, DIS, Feza, UWC Arusha, UWC Moshi, St Constantine, Arusha Meru, Rafiki, Academic International School, Isamilo, ISZ.