Onyango, Kahata wawafunika Chama, Bwalya

TIMU ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' iliyokuwa na wachezaji wawili kutokea Simba, Joash Onyango na Francis Kahata imeibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya timu ya taifa ya Zambia 'Chipolopolo' katika mechi iliyochezwa jana, Oktoba 9, Uwanja wa Nyayo nchini Kenya.

Wachezaji hao wawili nyota wa Simba, Onyango na Kahata wamewafunika wenzao wanaocheza nao klabu moja, Clatous Chama na Larry Bwalya ambao wote hawakufanikiwa kujiunga na timu  kwa sababu mbalimbali.

Chama ambaye alijumuishwa katika kikosi cha Chipolopolo na kocha, Merbian Milutin Sredojevic 'Micho' alichelewa kufika kwenye muda sahihi nchini Zambia na kusababisha kocha huyo kuondoa jina lake kikosini huku Chama mwenyewe akijiteta kwamba  hakukuwa na mpangilio sahihi wa tiketi ya ndege ambayo alitumiwa ili kwenda kujiunga na wenzake.

Wakati Bwalya na Chama wakikwama na kuendelea kuwepo nchini hadi sasa Onyango aliyecheza dakika zote 90, katika kikosi cha Harambee Stars na Kahata aliyeingia dakika 79, kuchukua nafasi ya Kenneth Muguna mambo yalikuwa mazuri kwao kwa kuwa wote walionesha viwango vikubwa.
 
Kikosi cha Harambee Stars kilianza na kipa, Ian Otieno, Baraka Badi, David Owino, Onyango, Brian Mandela, Anthony Akumu, Muguna/ Kahata, Lawrence Juma, Erick Johanna, Cliff Nyakeya na Masud Juma.

Wakati wapinzani wao Zambia walianza na Sebastien Mwange, Lubambo Musonda, Zacharia Chilongoshi, Tandi Mwape, Chongo Kabaso, Benson Sakala, Kelvin Kapumbu, Edward Chilufya, Kings Kangwa, Evans Kangwa na Fashion Sakala

Mechi nyingine kali ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na Watanzania wengi ni mpinzani wa Taifa Stars katika mechi ya kwanza ya kufuzu mataifa Afrika (Afcon), Tunisia ambao walikuwa nyumbani na walishinda mabao 3-0, dhidi ya Sudan

Mabao yao yalifungwa na Eddine Khaoui, Ali Maaloul na Ben Slimane, Tunisia itacheza na Taifa Stars mechi ya kufuzu Afcon kati ya Novemba 9-17 mwaka huu.

Mechi nyingine ambazo zilichezwa Oktoba 9, Japan ilitoka suluhu na Cameroon, Burkina Faso ilishinda 3-0, dhidi ya DR Congo ambayo kocha wake msaidizi ni Mwinyi Zahera ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa ufundi katika kikosi cha Gwambina.

Gambia ambayo imemuajiri kocha wa viungo wa Yanga (Riedoh Berdien), kuweka sawa miili ya wachezaji wa taifa hilo ilishinda1-0, dhidi ya Congo, Ghana ilifungwa 3-0, na Mali, Meuritania ilishinda 2-1 na Sierra Leone, Morocco ilishinda 3-1 dhidi ya Senegal wakati Nigeria ilifungwa bao 1-0 na Algeria.