Ondoka tu.. Pogba apewa makavu Man United

MANCHESTER ENGLAND. WE nenda tu. Gwiji la Manchester United, Paul Ince amemwambia kiungo Paul Pogba “ondoka” ikiwa ni wiki chache tu zimepita tangu supastaa huyo wa Ufaransa kukiri ndoto zake ni kwenda kuichezea Real Madrid.

Kiungo Pogba aliendelea kusugua benchi wikiendi iliyopita kwenye mchezo ambao Man United ilitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Chelsea wa Ligi Kuu England.

Kwenye mchezo huo, Kocha Ole Gunnar Solskjaer aliamua kuwaanzisha Fred na Scott McTominay kwenye kiungo ya kuzuia huku Bruno Fernandes akisimama mbele yao.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia, Pogba aliingizwa kipindi cha pili dakika ya 58 alipochukua nafasi ya fundi wa mpira wa Kihispaniola, Juan Mata.

Lakini, Ince anaamini huu ni wakati mwafaka kwa Pogba kuachana na maisha ya Old Trafford.

Akizungumza na beIN Sports, Ince alisema: “Kwake yeye kuendelea kukaa kwenye benchi na kuwa mtazamani ni kumkosea heshima, McTominay na Fred playing kucheza kwenye nafasi yake, ningependa kusema, ‘Ningefanya kosa kubwa sana kama nashindwa kuingia kwenye timu’.

“Nafahamu amekuwa na majeruhi na anaweza kumwingiza kwenye mechi baadaye, lakini nadhani ni wakati wake wa kuondoka.

“Alijitokeza wiki mbili zilizopita na kusema anataka kwenda kujiunga na Real Madrid.

“Nadhani kiwango chake, tangu alipokuwa kwenye timu hiyo, kimekuwa cha kupanda na kushuka.

“Paul Pogba ni mchezaji wa kiwango cha dunia na alipokuja Old Trafford, nilidhani ingekuwa vizuri sana. Lakini, kile ambacho amekuwa akifanya ni matatizo tu.

“Mashabiki wamekuwa wakimkosoa sana na sasa amekuja Bruno Fernandes ameonyesha yeye ndiye mchezaji ambaye Manchester United inahitaji kuwa naye.”

Siku chache kabla dirisha la usajili kufungwa mapema mwezi huu, Pogba alisema ndoto zake ni siku moja kwenda kuichezea Real Madrid.

Pogba alisema: “Ndio, wanasoka wote wangependa kuichezea Real Madrid. Pengine ni ndoto. Ni ndoto kwangu, kwa nini isiwe siku moja?

“Nikiwa nasema hayo, mimi ni mchezaji wa Manchester United na naipenda klabu yangu.”

Pogba ameripotiwa kujitoa kwenye soka la kimataifa baada ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kudai Uislamu ni chanzo cha ugaidi wa kimataifa.

Staa huyo wa Man United ameripotiwa kufanya uamuzi huo kutokana na kauli ya kiongozi wa nchi yake aliyotoa Ijumaa iliyopita kwa mujibu wa vyanzo vya habari wa Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, Pogba amesema jambo hilo sio kweli na hajawahi kusema kokote.