Omog afunguka kilichomwondoa Simba

Muktasari:

Baada ya aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma kuondolewa ndani ya kikosi hicho chenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi amesema, aliwahi kuambiwa na wachezaji awe makini naye kwa sababu alikuwa anautaka ukocha mkuu Simba.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog amekiri aliwahi kuambiwa na wachezaji kuwa awe makini na Mrundi Masoud Djuma.
Omog ambaye kwa sasa yuko nyumbani kwao Younde, Cameroon mapumzikoni amedai wachezaji hao walimwambia Djuma anataka kazi ya Kocha Mkuu Simba.
"Sijui lililompata Masoud na huyo, Mbelgiji (Patrick Aussems) lakini binafsi baadhi ya wachezaji walinifuata na kunambia maneno hayo,"alisema Omog.
Djuma amefutwa kazi mwanzoni mwa wiki hii na ameshaondoka jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa hakuwa na maelewano mazuri na mkuu wake Aussems.
Hata hivyo, awali Djuma alikaririwa akisema kuwa hakuwa anaitaka nafasi ya ukocha mkuu Simba kama ilivyokuwa inadaiwa isipokuwa ni maneno ya watu wenye nia mbaya na yeye.