Ommy Dimpoz atoa picha yake akiwa ICU

Thursday September 13 2018

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Leo Septemba 13, 2018 ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya msanii Ommy Dimpoz, katika ukurasa wa mtandao wake wa Instagram ameweka picha zake zilizopigwa alipokuwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) nchini Afrika Kusini.

Katika picha hizo ameandika waraka mrefu wa shukrani akielezea safari yake ya miezi mitano katika matibabu ya koo katika nchi za Kenya na Afrika Kusini, kabla na baada ya kufanyiwa upasuaji.

Amemtaja meneja wake, Christine Mosha maarufu kama Seven kuwa katika kipindi hicho alisimama kama mama yake katika kumuuguza.

“Shukrani za dhati my lovely manager (mpendwa meneja wangu) Seven ambaye amehangaika na mimi mfano wa mama mzazi na mtoto wake,” amesema.

Mwingine aliyemtaja katika waraka huo ni Gavana wa Jimbo la Mombasa, Kenya, Hassan Joho kwamba amemuuguza katika kipindi chote cha matibabu kuanzia Kenya na Afrika Kusini.

Katika waraka wake huo ameelezea namna alivyokata tamaa ya kuishi baada ya hali yake kuwa mbaya, lakini alipata nguvu baada ya kumuona mgonjwa aliyekuwa mahututi pembeni yake akipona.

“Kuna kipindi wakati nimelazwa nilikata tamaa ya kuishi nikaona labda muda wangu umekwisha lakini hapo hospitali akaletwa mgonjwa mwingine ambaye alikuwa pembeni yangu,” amesema.

“Alikuwa ameshambuliwa na majambazi kwa risasi tisa mwilini lakini madaktari wakafanikiwa kuokoa maisha yake na akapona sasa nikajiuliza mimi ni nani nikate tamaa ya kuishi na nikajifunza kwamba kuugua si kufa.”

 

Advertisement