Olunga ajiunga na Gyan mkekani

Thursday March 14 2019

 

By Vincent Opiyo

 

STRAIKA Michael Olunga ataukosa mchuano wa Harambee Stars baina ya Ghana wa kufuzu fainali za kombe la mataifa bora barani (AFCON) Jumapili ya Machi 23 kwa sababu ya jeraha.

Olunga alipata jeraha la uvundo wa paja kwenye mechi aliyofunga bao la ushindi Jumamosi iliyopita dhidi ya Albirex Niigata kwenye ligi ya daraja la pili nchini Japan.

Anajiunga na nahodha wa Ghana Asamoah Gyan aliyetemwa kwenye kikosi chao kwa sababu ya jeraha.

Nafasi ya Olunga, ambaye amefunga mabao 17 kwenye mechi 34 akivalia jezi ya taifa, imetwaliwa na mshambulizi wa Zesco United Jesse Jackson Were.

Were mwanzoni aliwachwa nje ya kikosi cha kocha Sebastien Migne licha ya fomu yake nzuri nchini Zambia.

Japo hajafunga bao lolote kwenye mechi nyingi za Stars, Were anatarajiwa kupewa nafasi nyingine tena chini ya Mfaransa huyu kuonyesha umahiri wake.

Kikosi hichi kitaingia kambini Jumapili ijayo huku nyota wa kigeni wakitarajiwa kambini Jumanne. Kenya na Ghana tayari wamefuzu fainali hizi za nchini Misri kwanzia mwezi Juni japo Kenya inaongoza kundi F kwa pointi saba, moja mbele ya Ghana.

Advertisement