Olunga: Tunaiheshimu Ethiopia, hatuwezi kufanya makosa

Muktasari:

Harambee Stars inaongoza Kundi F, ikiwa na pointi nne, na endapo itashinda mchezo wa Jumapili, itakuwa ni nafasi nzuri ya kuanza kuota ndoto za kuelekea Cameroon, kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 14.

Nairobi, Kenya. Baada ya kufanikiwa kulazimisha sare ya 0-0 ugenini katika mchezo wa tatu wa kundi F, kusaka tiketi ya kushiriki kombe la mataifa Afrika, Harambee Stars itashuka uwanjani siku ya Jumapili, kucheza mchezo wa marudiano, utakaopigwa ugani Moi Kasarani, kuanzia saa 10, alasiri.

Kuelekea mchezo huo wa kukata na shoka, Straika wa zamani wa Girona FC, Michael Olunga, amewataka wachezaji wenzake kutowabeza Waethiopia na kusisitiza kuwa lazima wacheze kufa na kupona.

Akizungumzia mchezo wa kwanza, uliopigwa ugani Bahir Dar, Olunga alisema wenyeji wao walikuwa moto wa kuotea mbali na kama sio mbinu za Kocha Migne za kuwazuia Waaliya Antelopes, kitumbua cha Harambee Stars, inayoongoza kundi F, kingeingia mchanga.

 "Katika mchezo wa kwanza, niwe tu mweki kuwa tulitokea tundu la sindano. Ethiopia ni wazuri sana. licha ya kuwa Jumapili, tutakuwa nyumbani, hiyo sio sababu ya kuwabeza. Lazima tuwe makini sana,” alisema Olunga.

Kuhusu kitendo cha serikali kupitia wizara ya michezo kutangaza, kuondoa viingilio katika mchezo wa marudiano, Olunga anayekipiga katika klabu ya Kashiwa Raysol, aliipongeza serikali na kuwataka kuendelea kuisapoti Stars.