Oliech akinukisha Gor Mahia, kisa...

Wednesday February 27 2019

 

Mabosi wa straika mkongwe Dennis Oliech wameitaka klabu ya Gor Mahia kumlipa mchezaji huyo mkwanja wake.

Oliech alisusia mechi dhidi ya Walgeria Hussein Dey juzi Jumamosi baada ya Gor kutomlipa fedha za usajili kulingana na makubaliano ya kimkataba.

Straika huyo aliyerejea uwanjani Januari mwaka huu baada ya kutangaza kustaafu miaka miwili iliyopita, alichukua uamuzi huo  alipokuta  kawekewa fedha ambazo hazitoshi kwenye akaunti yake ya benki.

Sasa katishia kutoichezea Gor kabisa kama hawatamlipa Sh3 milioni ambazo  walikubaliana kama kiwango chake cha fedha za usajili.

Kulingana na ajenti wake ambaye pia ni kakake mkubwa Ken Oliech, aliyefanikisha dili hiyo, mdogo wake hatahudhuria kikao chochote cha mazoezi ya Gor mpaka pale atakapolipwa.

Ken kasema kuwa Gor ilishindwa kutimiza ahadi ya mkataba wake toka Disemba mwaka jana.

“Wajua toka Oliech aliposainiwa na klabu Disemba, hajalipwa hata shilingi ya fedha za usajili tulizoafikiana na muda wote amekuwa akicheza,” Ken kafunguka.

Ken pia kafichua kwamba  kwenye hatua za awali za mazungumzo, waliipendekezea klabu kwamba walitaka Oliech aitumikie klabu kama mchezaji huru ili asiwe akilipwa mshahara wowote zaidi ya marupurupu.

Hata hivyo uongozi wa klabu ukasisitiza umsajili na ndipo wakaafikiana kiasi cha Sh3 milioni kama fedha za usajili.

Kwa kutia sahihi mkataba, ina maana kuwa Oliech hawezi kuondoka klabuni kiulaini bila mvutano.

Fedha hizo za usajili zilitakiwa kulipwa mdogo mdogo, awamu ya kwanza ikiwa ni baada ya miezi mitatu lakini mpaka leo hamna kitu.

Ken aidha kaweka mambo sawa kwa kusema ishu ya Oliech haipo kwenye mshahara kwa sababu wanaelewa kuna wakati inaweza kuchelewa ila ni kwenye fedha za usajili ndio wana tatizo nao.

 

 

Advertisement