Ole sasa aomba msaada

Muktasari:

Jana Jumatano usiku, Man United ilitarajia kumenyana na Burnley kwenye Ligi Kuu England na kocha Solskjaer anatafuta mtu wa saikolojia kuwatibu wachezaji wake ili kutokuwa na tabia hiyo ya kubagua mechi.

MANCHESTER, ENGLAND . KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer anatafuta mtaalamu wa saikolojia kwenye michezo kwenda kutibu vichwa vya wachezaji wake kutokana na matokeo ya hovyo wanapokabiliana na timu ndogo.

Solskjaer anaamini kuna tatizo sehemu linalowakabili wachezaji wake wanapocheza na timu ndogo kwa sababu viwango vyao vinakuwa tofauti na wanaposhuka uwanjani kuzikabili timu vigogo.

Jambo hilo linamtia shaka kocha huyo akisema kwenye mechi kubwa, mastaa wake wanawasha moto kwelikweli, lakini wanapocheza na timu zinazopambana zisishuke daraja, wanakuwa hovyo uwanjani na kupoteza kirahisi sana.

Jana Jumatano usiku, Man United ilitarajia kumenyana na Burnley kwenye Ligi Kuu England na kocha Solskjaer anatafuta mtu wa saikolojia kuwatibu wachezaji wake ili kutokuwa na tabia hiyo ya kubagua mechi.

Man United ndiyo timu pekee iliyogawana pointi na Liverpool msimu huu huku wakiwachapa pia Manchester City uwanjani kwao Etihad. Wamezichapa timu ngumu pia za Leicester City, Chelsea mara mbili — 4-0 kwenye Ligi Kuu England na 2-1 kwenye Kombe la Ligi na wakiwachapa pia wasumbufu Wolves. Lakini, utashangaa imechapwa na Watford, Bournemouth, West Ham, Newcastle na Crystal Palace — wakitoka sare pia na Aston Villa.

Jambo hilo linamfanya kocha Solskjaer kushindwa kuielewa timu yake na hivyo sasa anahitaji msaada wa nje kuja kurekebisha mambo.

Man United waliichapa Burnley 2-0 uwanjani Turf Moor mwezi uliopita, lakini walihitaji mabao mawili ya dakika za mwisho kupata sare nyumbani msimu uliopita.

Solskjaer alisema: “Kila wakati tunapocheza na Burnley shughuli inakuwa pevu. Wanakuwa wasumbufu uwanjani utashani wameshinda mechi tano mfululizo.”