Ole apewa mikoba yote Man United

Muktasari:

  • Solskjaer amezidi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa kocha wa kudumu kwenye kikosi hicho kutokana na mwenendo wa timu hiyo inayofanya kwa sasa, ambapo hadi anafika mechi ya jana Jumapili dhidi ya Leicester City kwenye Ligi Kuu England kikosi chake kilikuwa hakijapoteza mechi yoyote.

MANCHESTER, ENGLAND.MANCHESTER United imeelezwa kwamba itamwaamini kocha Ole Gunnar Solskjaer na kuamua nani wa kusajiliwa kwenye kikosi hicho hata kama hatapewa kibarua cha kudumu huko Old Trafford.

Kocha huyo wa muda atahusika kwa kila kitu katika kuwatambua wachezaji wanaopaswa kusajiliwa na Man United hata kama kibarua chake hicho kitachukuliwa na Mauricio Pochettino mwishoni mwa msimu.

Solskjaer alisema: “Napaswa kutambua kiwango cha mchezaji, ametoka wapi na anaweza kubadilika kwa ajili ya klabu. Hilo ndilo tunalotaka kulitazama zaidi hasa kwa miaka ijayo, kuona ni aina gani ya wachezaji tunaw owahitaji na kuwataka. Tunataka wachezaji wenye damu ya kuichezea Man United.”

Solskjaer amezidi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa kocha wa kudumu kwenye kikosi hicho kutokana na mwenendo wa timu hiyo inayofanya kwa sasa, ambapo hadi anafika mechi ya jana Jumapili dhidi ya Leicester City kwenye Ligi Kuu England kikosi chake kilikuwa hakijapoteza mechi yoyote.

Na kilichoelezwa ni kwamba wamiliki wa klabu hiyo wamepanga kutumia Pauni 200 milioni kwenye usajili wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Solskjaer alisema: “Klabu hii siku zote itapata ushauri wangu kama wataniuliza. Hilo ni jambo la kawaida tu. Yeyote atakayekuwa kwenye benchi kwa sababu ndiye atakayehusika na wachezaji.”