Ole anajiamini, atamnasa Sancho

Muktasari:

Sambamba na hilo, Man United wanamtaka pia kiungo Christian Eriksen, licha ya kwamba staa huyo wa Denmark anataka kwenda Hispania, Tottenham Hotspur wao wanapanga kumpiga bei Januari kuliko kusubiri hadi mwisho wa msimu akaondoka bure.

DORTMUND, UJERUMANI . JADON Sancho anasakwa kila kona huko Ulaya licha ya kwamba Borussia Dortmund hawataki kumpiga bei supastaa wao huyo Mwingereza kwenye  dirisha la Januari.
Staa huyo anahusishwa na timu kibao, lakini Manchester United wao wanaamini ndio waliokwenye nafasi bora zaidi ya kukamilisha dili na Dortmund kwa ajili ya kunasa huduma ya mchezaji huyo.
Sambamba na hilo, Man United wanamtaka pia kiungo Christian Eriksen, licha ya kwamba staa huyo wa Denmark anataka kwenda Hispania, Tottenham Hotspur wao wanapanga kumpiga bei Januari kuliko kusubiri hadi mwisho wa msimu akaondoka bure.
Timu nyingine zinazomtaka Sancho ni Manchester City na Chelsea, huku Liverpool waliokuwa wakitajwa kwamba wapo kwenye mbio, wanaonekana pengine wasiingie kwenye vita hiyo baada ya kufanikiwa kumnasa Takumi Minamino kutoka RB Salzburg.
Mapema wiki hii, kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer alisema tena kwa msisitizo kwamba Old Trafford pataendelea kuwa kivutio kwa wachezaji wenye majina makubwa duniani, akisema: “Mnasema mawakala hawataki kuleta wachezaji wao hapa, nnina hakika wanapenda sana waje kwetu. Sizungumzi na mawakala wengi kwa kusema ukweli, ila Man United ni klabu kubwa duniani, hivyo wachezaji wengi wanataka kuja hasa katika kipindi hiki cha kufanya mapinduzi ya kujijenga upya.”
Sancho amekuwa na wakati mgumu huko Dortmund akikabiliwa na mambo kadhaa ya kinidhamu yanayomfanya alipishwe faini na kuwekwa benchi kwenye mechi kadhaa.