Okwi pasua kichwa

Monday January 14 2019

 

By Thobias Sebastian

ACHANA na mpira mwingi alioupiga juzi Jumamosi kwenye pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, unaambiwa straika Emmanuel Okwi ameivuruga Simba na kuwafanya mabosi wake kuanza kuhaha kuweka mambo sawa.

Okwi aliyeifungia Simba bao la kwanza kwenye mchezo huo kabla ya kutengeneza mengine mawili yaliyowekwa kimiani na Meddie Kagere wakati wakiizamisha JSS Saoura ya Algeria mabao 3-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Uwanja wa Taifa, amewavuruga mabosi kutokana na kutaka kutimka zake Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, huku pia akitakiwa na timu nyingine ya Misri ambayo hawakutaka kuitaja.

Mabosi wa Simba presha inawapanda kwa vile straika huyo mkataba wake upo ukingoni ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu na wanahofu kubwa namna ya kumgusia juu ya kumuongezea mkataba kwani huenda akawapandishia dau ambalo hawatalimudu kwa sasa.

Ofa hizo mbili moja iliyokuja ghafla juzi usiku baada ya straika huyo kuupiga mwingi na kuivutia moja ya klabu kutoka Misri waliotuma maombi ya kutaka kumchukua ili akakipigie nchini humo.

Mwanaspoti imenasa taarifa kwamba mara baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya JS Saoura kuna timu kubwa moja ya Misri ilituma maombi ya kumtaka Okwi na kama Simba watakuwa tayari wakae mezani kuongea dili ili kufikia muafaka wa kumnasa nyota huyo kutoka Uganda.

“Kuna timu kubwa tu kutoka Misri imetuma maombi mara baada ya kumaliza mechi yetu na JSS walionekana walikuwa wanamfuatilia muda mrefu na kipimo kilikuwa kumuona katika mechi ya juzi ambayo kiukweli alikuwa katika kiwango bora,” kilidokeza chanzo kutoka Simba.

“Baada ya kufika maombi haya kwetu imetuvuruga kwani tunashindwa kukaa na Okwi mezani mapema yote hii anaweza kutaka kiasi kikubwa ili aweze kusaini mkataba mpya, kutokana mkataba wake wa sasa kuelekea ukingoni.

“Tunafahamu fika tunatakiwa kujipanga ili kumbakisha Okwi hapa Simba kutokana na ofa hizi mbili za Misri na Kaizer Chiefs kuwa na pesa nyingi ambazo wameweka mezani na kumtaka mchezaji wetu, kwa sasa tumechanganyikiwa juu yake, ila tunaimani tutaongea nae ili akubali kusaini mkataba mwingine hapa kwetu.

“Mwenyewe ameonekana kutaka kwenda Kaizer kama tutashindwa kumbakisha, ila ishu ni kwamba akiguswa kwa sasa anaweza kudai dau kubwa kwani mipango yetu ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa ambayo tumeanza vyema na mashabiki pamoja na viongozi wamekuwa na furaha kutokana na matokeo ya juzi.”

Alipoulizwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hawana mpango wa kumuuza mchezaji yoyote aliyekuwa katika kikosi chao kwani wao malengo yao ni kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu.

“Ili tuweze kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa ya Afrika lazima tuwe na wachezaji waliokamilika, kwa maana hiyo hatuna mpango wa kuuza mchezaji yoyote kwa sasa ili kuweza kufikia yale malengo ya timu ambayo tumepanga,” alisema.

“Nimesikia kuna ofa zililetwa si kwa Okwi tu bali hata John Bocco na Meddie Kagere kutoka katika timu nyingine lakini si dhani kama kutakuwa na uwezekano wa kumuachia mchezaji yetu yoyote,” alisema Try Again ambaye alikuwa Kaimu Rais katika uongozi uliomaliza muda wake.

WAARABU WAIPA MAMILIONI SIMBA

Katika hatua nyingine, imefahamika kuwa pambano lao dhidi ya Waarabu, limeipa Simba mkwanja wa maana hasa baada ya mabosi wa klabu hiyo kuweka tiketi maalum za Sh 100,000 zilizowapa ofa maalum kwa waliokata na kuifanya klabu hiyo ivune mamilioni.

Tiketi hizo za Platinum zilikuwa zikiwapa ofa watazamaji kwenda hoteli ya Serena na kuchukuliwa kwa usafiri maalumu ambayo uliwapeleka uwanjani na kuwarudisha hoteli mara baada ya mpira kumalizika huku wakisindikizwa na msafara wa polisi.

Mwanaspoti ilipata taarifa kuwa tiketi hizo 120 zote ziliuzwa na kwa maana hiyo, klabu ilivuna jumla ya Sh 12 Milioni, huku mapato yote yakiwa ni kiasi cha Sh 195 milioni.

Kwa waliokata tiketi hizo walipata huduma ya kunywa na kula muda wote uwanjani na kila mmoja alipewa uzi wa klabu hiyo ya Simba, huku wakibebwa katika mabasi mawili kama ya kusafiria kwenda mkoani na wengine katika gari ndogo aina ya Coaster.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka Simba kiliidokeza Mwanaspoti kwamba mapato ya jumla kwa mchezo huo yamepatikana Sh195, japo Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara alipoulizwa ili kuthibitisha alidai hana taarifa na kueleza leo jumatatu atakuwa na mkutano na wanahabari.

“Aisee sina uhakika katika hilo, kwani sijafika ofisini, ila kesho (leo) saa 5 nitakuwa na mkutano na wanahabari, bila kufafanua kama atazungumzia suala la mapato yaliyotokana na mchezo huo au la!”

Advertisement