Okwi bado siku 10 tu

Thursday December 6 2018

 

By Khatimu Naheka

MASHABIKI wa Simba huenda wasiifurahie taarifa hii, lakini ukweli kuanzia sasa, straika wao Emmanuel Okwi ana siku tu kuwepo Msimbazi kabla ya kusepa zake Afrika Kusini kukipiga Kaizer Chiefs.

Kaizer wanamtaka Okwi, baada ya mchezaji huyo kuonekana kutaka kubadilisha mazingira ya soka lake, huku ikitajwa ishu ya mshahara aliokatwa Julai mwaka huu ndio tatizo la straika huyo kutaka kumtika Msimbazi.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa, Okwi ana ofa tatu za maana mezani kutoka Sauzi, lakini Bodi ya klabu ya Simba imeziambia klabu zote zinazopigana vikumbo kumnyakua Mfungaji Bora huyo wa msimu uliopita nio kufanya haraka kumalizana nao kabla ya dirisha la usajili kufungwa siku 10 zijazo.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, aliliambia Mwanaspoti kuwa mezani kwake kuna ofa tatu za Okwi kutoka Afrika Kusini.

Alisema katika ofa hizo ni ofa moja ndio inayoonekana kuwa ya uhakika na tayari klabu yao imeshawapa kitu inachokitaka ili kuwapa mchezaji huyo mwenye mabao saba katika Ligi Kuu ya msimu huu na bao moja la mechi za kimataifa.

Magori alisema ameiambia klabu hiyo kuwa wanatakiwa kwanza wanatakiwa kuleta ofa hiyo kimaandishi baada ya wao kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na bodi yao.

“Tumepokea hizo ofa za Okwi, tumefanya maongezi na klabu tatu zinazomtaka, ila kati ya hizo ni moja tu tunaona wana dhamira ya kweli kumhitaji,” alisema.

“Tumewaambia tunataka waje kwa maandishi sasa lakini pia wafanye haraka kabla ya kufika Desemba 15 wakati ambao usajili wetu wa ndani utafungwa ili Simba nayo iweze kupata mchezaji mwingine.”

Magori alisema Simba haina tabia ya kumzuia mchezaji kuondoka, hivyo hata kama klabu zinazomtaka zitatekeleza haitakuwa na tatizo, huku chanzo makini kikisisitiza kuwa, Okwi anatakiwa zaidi na Kaizer kama Mwanaspoti lilivyoripoti.

Ishu nzima ni hii

Inaelezwa kuwa, Okwi ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu anataka kuondoka baada ya kubaini ufalme wake Msimbazi umepoteza tangu aje Meddie Kagere, lakini pi ni kukerwa na kukata mshahara.

Inadaiwa Okwi, Juuko Murshid na Haruna Niyonzima walikatwa mshahara kwa kuchelewa kambi, kitu kilichomuudhia straika huyo wa kimataifa wa Uganda na ndio maana amekuwa akishinikiza kuondoka Msimbazi. Okwi, ambaye ameiwezesha kuipa Simba kubeba ubingwa msimu uliopita baada ya kutoka kapa kwa misimu mitano mfululizo, hana furaha klabuni hapo tangu akumbwe na adhabu hiyo.

“Kosa hilo lilitukera kama uongozi, kwani alitakiwa kurudi nchini kwa muda baada ya majukumu yake ya timu ya taifa, lakini alichelewa kurudi bila sababu ya msingi na uongozi uliamua kumkata mshahara wa mwezi mmoja ili iwe funzo kwa wengine,” mmoja wa kigogo wa Simba alilidokeza Mwanaspoti.

Hata hivyo, inaelezwa ofa ya dau nono aliyotangaziwa na Kaizer Chiefs imemfanya straika huyo kutaka aruhusiwe atimke zake Afrika Kusini na kama ataondoka itakuwa ni mara ya tatu kwake kuingia na kutoka Msimbazi tangu alitua mara ya kwanza 2009.

Kessy anarudi

Ushindi wa bao 1-0 wa Nkana FC dhidi ya UD Songo, sasa timu hiyo itakutana na Simba katika mchezo wa kwanza utakaopigwa Zambia.

Hassan Kessy, beki wa zamani wa Simba na Yanga anayekipiga Nkana atarejea nchini kupambana na timu yake ya zamani.

Advertisement