Okwi amngoa kigogo Simba

UAMUZI wa kumruhusu mapema straika Emmanuel Okwi kujiunga na timu yake ya taifa ya Uganda, umemponza Meneja wa Simba, Robert Richard aliyekumbana na rungu la Shirikisho la Soka nchini (TFF) lililomfungia sambamba faini ya Sh4 milioni.

BY CHARLES ABEL

IN SUMMARY

  • Kuruhusiwa kwa Okwi kuiwahi Uganda, huku nyota sita wa Simba, John Bocco, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Said Ndemla na Shiza Kichuya wakishindwa kuwahi kambi ya Taifa Stars, kimemfanya Richard kufungiwa mwaka mmoja na faini hiyo kwa kufanya hujuma kwa timu ya taifa. Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Wakili Hamidu Mbwezeleni alisema jana, Richard amepewa adhabu hiyo baada ya kamati kumkuta na makosa mawili ya kukiuka maadili kama kiongozi wa soka.

Advertisement

UAMUZI wa kumruhusu mapema straika Emmanuel Okwi kujiunga na timu yake ya taifa ya Uganda, umemponza Meneja wa Simba, Robert Richard aliyekumbana na rungu la Shirikisho la Soka nchini (TFF) lililomfungia sambamba faini ya Sh4 milioni.

Kuruhusiwa kwa Okwi kuiwahi Uganda, huku nyota sita wa Simba, John Bocco, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Said Ndemla na Shiza Kichuya wakishindwa kuwahi kambi ya Taifa Stars, kimemfanya Richard kufungiwa mwaka mmoja na faini hiyo kwa kufanya hujuma kwa timu ya taifa. Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Wakili Hamidu Mbwezeleni alisema jana, Richard amepewa adhabu hiyo baada ya kamati kumkuta na makosa mawili ya kukiuka maadili kama kiongozi wa soka.

“Kosa la kwanza ni kuihujumu timu ya taifa kwa kutowapa wachezaji taarifa sahihi za kujiunga na kambi jambo lililosababisha wachelewe, huku kosa la pili likiwa ni kutotii amri na maagizo halali kutoka kwa mamlaka zilizo juu yake.

“TFF ilifanya mawasiliano na viongozi wa Simba ambao ni mwenyekiti na katibu kupitia barua na kwa nyakati tofauti walimwagiza huyu bwana meneja wa timu kuhakikisha wachezaji wanajiunga na kambi ndani ya muda uliopangwa.

“Yeye hakufuata maelekezo ambayo alipewa na badala yake akamsikiliza kocha ambaye tayari alishawaruhusu wachezaji kwenda mapumziko siku mbili wakati kimsingi yeye ndiye mwenye mamlaka kuliko kocha.

“Sasa kutokana na hilo, kamati kwa kuzingatia kanuni za maadili za kwa viongozi wa soka, inampa adhabu ya kumfungia kutojihusisha na soka kwa mwaka mmoja sambamba na faini ya Sh4 milioni, kila kosa lina adhabu yake hivyo tumeunganisha.”

Mbwezeleni alisema kitendo cha Richard kumruhusu Okwi ni sawa na kuihujumu kwa timu ya taifa, hivyo kamati yake isingeweza kumvumilia.

“Ameleta mgongano wa kimaslahi baina ya Simba na TFF. Kilichoshangaza zaidi aliweza kumruhusu mchezaji wa Uganda kwenda kujiunga na timu yake tena kwa kupigiwa simu tu, ikumbukwe Taifa Stars na Simba waliweka kambi sehemu moja.”

Hata hivyo, Richard alivyoulizwa juu ya adhabu aliyopewa alisema hawezi kusema chochote kwa sasa.

KISIWA CHUPUCHUPU

Katika hatua nyingine Kamati hiyo ya maadili imeshindwa kumwadhibu Kaimu Katibu wa Simba, Hamis Kissiwa baada ya kuonekana hana hatia ya makosa aliyotuhumiwa.

Kisiwa na Robert walipelekwa mbele ya kamati hiyo kwa pamoja kutokana na sakata hilo, ila ameonekana hakuhusika kuchelewesha nyota wa Simba kambini.

“Katibu wa Simba alitimiza kwa ufasaha majukumu yake hivyo kamati haijamtia hatiani,” alisisitiza Mbwezeleni.

SIMBA YAONYWA

Wakati huo huo TFF imeionya Simba na klabu nyingine zote ikizitaka kufuata taratibu za kikanuni pindi wanapoialika timu kutoka nje ya nchi kuja hapa Tanzania kucheza mechi ya kinataifa ya kirafiki.

“Tumewaandikia barua wanachama wetu ambao ni klabu na vyama vya mkoa tukiwajulisha wanapaswa kufuata taratibu kabla ya kuleta timu kutoka nje ya nchi kwa sababu mara kwa mara wamekuwa hawafanyi hivyo jambo linaloweza kuleta matatizo siku za usoni.

Tumeamua kutoa angalizo juu ya hili kwa sababu hivi karibuni tumeshuhudia timu za AFC Leopards na nyingine kutoka Kenya zimekuja nchini kucheza mechi za kirafiki dhidi ya timu za Simba na Biashara United.

Madadi alisema ili timu ya nje ije kucheza mechi ya kirafiki ni lazima kuwe na kibali kutoka Fifa, kibali kutoka TFF na shirikisho au chama cha soka kwa nchi ambayo klabu husika inapotokea kuja nchini.

More From Mwanaspoti
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept