Okwi aipasua kichwa Simba

Muktasari:

  • Okwi alisaini miaka miwili akitokea SC Villa ya Uganda, timu iliyomlea na kumkuza kisoka, hivyo kama ataondoka bure ni wazi Simba itapishana na mamilioni ya fedha kizembe.

MABOSI wa Simba wanahaha ili kusaka dawa ya kuimaliza TP Mazembe katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini nyota wao Emmanuel Okwi akiiendelea kuipasua kichwa klabu hiyo kwa sasa.

Kama hujui tu ni kwamba, Okwi ndiye mchezaji pekee aliyeiingizia klabu hiyo pesa ya maana kutokana na mauzo yake kwa klabu mbili tofauti, ila safari hii huenda akatimka klabuni hapo bila kuipa hata senti moja.

Mauzo ya Okwi anayetokea Uganda yameipa Simba jumla ya Dola 410,000 (zaidi ya Sh 946 milioni) kwani kwanza ilivuna Dola 300,000 mwaka 2013 ilipomuuza Etoile Du Sahel ya Tunisia kabla ya kuvuna dola nyingine 110,000 aliponyakuliwa na klabu ya Sonderjyske ya Denmark.

Ishu ya sasa ilianzia mwaka jana wakati Kaizer Chiefs ya Ligi Kuu Afrika Kusini ilipotaka kumnunua, ila dili hilo likafa baada ya Simba kutaka ilipwe Dola 150,000 (zaidi ya Sh 300 milioni) na Wasauzi kuamua kuwachunia kimtindo.

Lakini juzi kati imefahamika, Kaizer Chiefs imerejea na kumhitaji Mganda huyo, ila kwa kusubiri amalize mkataba wake Msimbazi mwishoni mwa msimu huu.

Okwi alisaini miaka miwili akitokea SC Villa ya Uganda, timu iliyomlea na kumkuza kisoka, hivyo kama ataondoka bure ni wazi Simba itapishana na mamilioni ya fedha kizembe.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mshambuliaji huyo mwenye mabao saba Ligi Kuu kuondoka Simba bila kuipa pesa, kwani pesa yote ya Kaizer itaenda kwake ikiwamo fedha za usajili kwani atakuwa huru.

Okwi amekuwa akitoka na kuingia ndani ya Simba ukiliganisha na wachezaji wengine ambao Simba wamewahi kuwauza ama kuachana nao na kwenda kutafuta timu nyingine nje ya nchi.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema uwezekano wa kumpa mkataba mpya Okwi ni mdogo ingawa kuna mapendekezo ya kubaki.

“Ana mkataba na sisi hadi mwisho wa msimu huu, lakini maamuzi ya kubaki au kuondoka yapo mikononi mwa mchezaji, Okwi ni kama mtoto wetu hata akiondoka tutamruhusu na akitaka kurejea tutampokea itategemea na kiwango chake kwa wakati huo,” alisema Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

Mwanaspoti limebaini klabu nyingi za Sauzi hazipendi kuwanunua wachezaji kwa bei kubwa hivyo wapo tayari kuwasubiri wawe huru.

Hilo pia lilitokea kwa Abdi Banda anayeichezea Baroka FC ambapo alihitajika na timu za huko lakini alikwama kutokana na uongozi wa Simba kuhitaji pesa nyingi.

Banda aliondoka Simba bure na kujiunga na Baroka baada ya kumaliza mkataba wake na kuinyima Msimbazi fedha baada ya kulipwa zaidi ya Sh 200 milioni kwa mkataba wa miaka miwili.

Banda aliliambia Mwanaspoti; “Timu nyingi huku hazitaki kununua mchezaji akiwa na mkataba maana klabu huhitaji pesa nyingi sana ndio maana wanasubiri mchezaji amalizane na timu yake.

“Timu za Tanzania zikitaka kumuuza mchezaji zinataka pesa nyingi ila huku mchezaji akitaka kuondoka hakuna vizuizi na pesa wanayohitaji kama ana mkataba ni ya kawaida ambayo haiiumizi klabu nyingine na hata mchezaji.

“Huku wanajali sana maisha ya wachezaji na timu zao ndiyo faida wanayohitaji ni ndogo sana, huku ukiwa mchezaji huru huwezi kukosa timu ya kuichezea,” alisema Banda.

Ukichana na wachezaji hao wa Simba lakini mchezaji mwingine ambaye angeipatia pesa nyingi timu yake ni Himid Mao anayekipiga Misri.

Mao alikuwa mchezaji wa Azam FC kwa miaka yote na amekulia hapo lakini aliruhusiwa kwenda kutafuta maisha mengine nje ya nchi.

MSIMBAZI MTEGONI

Wakati ishu ya Okwi ikitikisa, Simba bado itakuwa kwenye majaribu mengine kama isiposhtukia mambo mapema kwani, mastaa wanane wa kikosi cha kwanza watakuwa huru mwishoni mwa msimu huu. Mastaa hao wanamaliza mikataba yao na bado mazungumzo ya kuongezewa mikataba hayajaanza.

Wachezaji hao ni Aishi Manula, Erasto Nyoni, John Bocco, James Kotei na Jonas Mkude. Pia, beki Mghana Asante Kwasi na Shomary Kapombe.

Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alisema Bodi ya Wakurugenzi inafahamu kuna baadhi ya wachezaji katika kikosi chao mikataba yao itamalizika msimu huu.

“Hakuna mchezaji yeyote tuliyempa mkataba wake wa kuitumikia Simba utakuwa umemalizika na tumempa ruhusa ya kuondoka kwa maana ya kwenda kujiunga na timu nyingine wote tuna mipango nao na tunaimani watasaini mikata mipya wa kubaki hapa.

“Bodi bado haijazungumza na mchezaji yeyote, ambaye mkataba wake unamalizika kutokana na majukumu ya mechi za kimataifa ambazo tunacheza mfululizo, lakini nadhani tutakaa nao na mambo yatakwenda sawa kwa pande zote mbili tutakubaliana,” alisema Mkwabi.

Katika hatua nyingine mabosi wa Simba wanaendelea kukuna vichwa wakishirikiana na benchi lao la ufundi ili kuona wanapenyaje kwenye mchezo wao wa marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe.

Simba itavaana na TP Mzembe Jumamosi jijini Lubumbashi, DR Congo baada ya wikiendi iliyopita kutoka suluhu jijini Dar es Salaam na Mkwabi alisema hawalali kwa sasa kufikiria namna ya kwenda kupindua meza ugenini, licha ya kutokuwa na rekodi ya kuvutia katika timu yao inapocheza mechi za ugenini kwenye michuano hiyo.