Okwi mchezaji bora, Pluijm kocha bora waiteka Ligi Kuu

Thursday November 8 2018

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Mkali wa mabao wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara (TPL) Oktoba msimu wa 2018-2019 huku Mholanzi Hans Pluijm wa Azam FC akiondoka na Tuzo ya Kocha Bora.
Okwi anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Yahya Zayd wa Azam na Eliud Ambokile wa Mbeya City alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Kwa mwezi huo Oktoba timu 18 zilicheza michezo mitano kila moja,  isipokuwa Simba na Yanga zilizocheza mechi nne.
Katika michezo hiyo minne ambayo Simba ilicheza, Okwi raia wa Uganda alitoa mchango mkubwa kwa kupata pointi 12,  kwa kushinda michezo yote na kumaliza ikiwa nafasi ya pili, huku Okwi akifunga mabao 7, kwa mwezi huo, matatu akifunga katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0.
Kwa upande wa Ambokile naye alitoa mchango mkubwa kwa Mbeya City kufanikisha kupata pointi 11, baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare miwili na kushika nafasi ya nane katika msimamo, akifunga mabao manne.
Kuhusu Zayd alitoa mchango mkubwa kwa Azam akifunga mabao matatu katika michezo mitano ambayo Azam ilicheza ikishinda yote na kupata pointi 15, ikishika nafasi ya kwanza.
Kamati ya Tuzo pia, imemchagua Kocha wa Azam FC, Han Pluijm kuwa Kocha Bora wa mwezi Oktoba akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa Mbeya City, Ramadhan Nsazwarimo.
Pluijm aliiongoza timu yake kupata pointi 15, baada ya kushinda michezo yote mitano iliyocheza na kushika nafasi ya kwanza, huku Aussems akiiongoza Simba kushinda michezo yote minne iliyocheza hivyo kupata pointi 12, na kushika nafasi ya pili, wakati Nsazwarimo alipata pointi 11 akishinda michezo mitatu na kutoka sare mitatu akiiwezesha timu yake kupanda hadi nafasi ya nane.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali, ambapo kwa ushindi huo Okwi atazawadiwa tuzo, king’amuzi kutoka Azam na Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.
Kwa upande wa makocha walioshinda tuzo hizo kwa msimu huu ni Amri Said wa Mbao FC aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Agosti na Mwinyi Zahera wa Yanga aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Septemba.