Okwi, Kagere wamharibia Mo

Friday November 9 2018

 

By OLIPA ASSA

MOHAMED  Rashid 'Mo Rashid' ni kati ya wachezaji watakaopelekwa kwa mkopo wakati wa dirisha dogo la usajili linalotarajia kufunguliwa Novemba 15 baada ya kushindwa kushindwa kutamba mbele ya washambuliaji wazoefu Emmanuel Okwi, John Bocco na  Meddie Kagere, yeye mwenyewe amefichua kitu kinachomnyima namba tangu ajiunge na Wanamsimbazi hao msimu huu.
Mo alilidokeza Mwanaspoti kwamba, alipotoka Prisons ambako alimaliza msimu wa 2017/18 akiwa na mabao tisa yaliowafanya Simba wavutiwe na huduma yake, hakujua kama angekutana na muziki mnene wa Okwi, Kagere na Bocco ambao ndio wanaoaminika mbele ya kocha Patrick Aussems.
Alisema uzoefu wa Okwi mwenye mabao (saba), Bocco (mawili) na Kagere (saba) ndio unaomnyima raha na kudai kuwa viwango vyao vipo moto kiasi kwamba kocha Aussems hawezi kuwaweka benchi, wakati anakimbizana na wapinzani wake kutaka kukaa kileleni  mwa msimamo wa ligi.
"Wepenzi wa Simba wanapaswa kujua kwamba sijafulia, ila nafasi ninayocheza kuna wachezaji wazoefu ambao wapo kwenye kiwango cha hali ya juu mfano Okwi na Kagere mpaka sasa wamechangia mabao 14 kila mmoja akifunga saba hayo ni nusu ya yale ambayo yanamilikiwa na timu nzima ambayo yapo 23.
"Kwa vyovyote kocha Aussems, hawezi kumwacha mchezaji ambaye tayari ana mchango mkubwa akaniingiza mimi, mechi zipo nyingi naamini nitacheza na kuonyesha kile nilicho nacho na mashabiki wataamini sijafulia bali ni changamoto ya viwango vya ushindani katika namba yangu,"alisema.
Mbali na Okwi, Kagere na Bocco kumpa changamoto ya namba, pia alikiri kukubalika na  Aussems ambaye alidai anakuwa anakaa naye na kumpa moyo kwamba ana kitu cha tofauti hapaswi kukata tamaa.
"Mara nyingi ananiambia nina kasi, pumzi na stamina, kuhusu kutonipanga ananiambia ukifika wakati atanipanga, kikubwa nifanye juhudi mazoezini kama vile nacheza katika kikosi cha kwanza,"alisema.
Beki kisiki wa zamani wa Simba,  Frank Kasanga 'Bwalya' alitoa somo kwa Mo Rashid kwamba kukosa namba kwake mbele ya wakongwe Okwi,  Bocco na Kagere kunategemeana na namna ambavyo anaichukulia thamani yake ya kazi.
"Lazima kutakuwa na mapungufu ambayo mchezaji ameyaonyesha kwa kocha mpaka kufikia hatua ya kushindwa hata kumpa dakika chache timu ikiwa imepata matokeo, kinachotakiwa ni mchezaji mwenyewe kutambua Simba inataka nini kwake na yeye kupandisha thamani yake.
"Akisema aondoke kwenda timu nyingine dirisha dogo, ataenda kufanya nini angali hajaonyesha chochote Simba, akijitathimini mwenyewe anaweza akabaki baadae akapata nafasi kama atajituma ama akaondoka kama anaona aendako atacheza,"alisema.
Kwa upande wa kocha Mlage Kabange alisema "Mo Rashid alipewa nafasi baadhi ya mechi lakini alishindwa kuonyesha kile kocha alikitegemea kwake, anachotakiwa kukifanya ni kuendelea kujituma kwa bidii kama vile yeye ndiye anameanza ndani ya kikosi cha kwanza," alisema

Advertisement