Okwi, Bocco waipandisha Simba nafasi ya pili ikiipumulia Yanga

Thursday April 25 2019

 

Saddam Sadick Mwanza. Timu ya Simba imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC FC kwenyemchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi (22) na John Bocco (83) na kuipeleka Simba kwenye nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 66.

Licha Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya KMC,lakini itajialaumu kwa nafasi zaidi ya mbili ilizopata na kushindwa kuzitumia vyema.

 Katika mchezo huo,KMC walitumia takribani dakika kumi kuonyesha makeke lakini baadaye waliweza kuzimwa ghafla.

Ilikuwa ni dakika ya 22 Straika Emanuel Okwi alipoiandikia Simba bao la kwanza akimalizia vyema mpira wa faulo wa James Kotei baada ya Yusuph Ndikumana kumchezea rafu John Bocco.

 Hata hivyo Bocco alikosa mabao ya wazi mawili ikiwa ya kwanza dakika ya 14 aliposhindwa kumalizia pasi safi ya Meddie Kagere,pia dakika ya 26 Clatous Chama shuti lake lilitoka nje na kama haitoshi tena Bocco akakosa bao lingine dakika ya 42 alipojikokota na mpira na shuti lake kutoka nje.

Advertisement

Hata hivyo KMC chini ya Kocha wake ,Ettiene Ndayiragije ilifanya mabadiliko mapema ya kumtoa Aron Lurambo na kuingia Kelvin Kijiri dakika ya 20.

Nahodha wa Simba, Bocco amesema wanajiandaa kwa ajili ya mchezo unaofuata na wanachoshukuru  ni kupata alama tatu.

Kwa ushindi huo, Simba imeikaribia Yanga ambayo ipo kileleni ikiwa na alama 74.

Advertisement