Oktay ataja maajabu ya Gor Mahia

Muktasari:

 

  • Gor ijilipanga na jitihada zake zilizaa matunda dakika ya 56, ilipopata penalti baada ya Boniface Omondi kuchezewa faulo ndani ya 18. Refa alipeana penalti iliyotiwa kimyani na straika Jaques Tuyisenge. Bao hilo liliipa nguvu Gor na ikaendelea kufanya mashambulizi ila bahati ya magoli zaidi haikusimama nayo licha ya kugonga mlingoti mara mbili.

KOCHA wa Gor Mahia, Hassan Oktay amebaki kushangaa jinsi kikosi chake kilivyofuzu hatua ya makundi na kutinga nane bora ya dimba la CAF Confederation Cup juzi Jumapili.

Oktay bado haamini ule uamuzi wa upendeleo wa refa wa kati haukutosha kuwavusha wapinzani wao Wakiwa wanavuta mkia wa Kundi D kwa alama sita, Gor walihitaji ushindi kwenye mechi yao ya mwisho dhidi ya Petro Atletico wa Angola.

Ikicheza nyumbani, Gor ilianza mchuano kwa mikosi, ikilishwa kadi mbili nyekundu pamoja na kocha wake.

Balaa ya kwanza iliiangukia katika dakika ya 36, kiungo mkabaji Ernest Wendo alipolishwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Vladanir Eston.

Dakika ya 44, beki Shaffiq Batambuze alionyeshwa kadi ya pili ya njano. Dakika 10 baadaye Kocha Oktay naye akalishwa kadi nyekundu.

Gor ijilipanga na jitihada zake zilizaa matunda dakika ya 56, ilipopata penalti baada ya Boniface Omondi kuchezewa faulo ndani ya 18. Refa alipeana penalti iliyotiwa kimyani na straika Jaques Tuyisenge. Bao hilo liliipa nguvu Gor na ikaendelea kufanya mashambulizi ila bahati ya magoli zaidi haikusimama nayo licha ya kugonga mlingoti mara mbili.

Hata hivyo, Gor ilihakikisha inadifendi vyema hadi dakika ya mwisho. Akizungumzia ushindi huo Oktay aliutaja kuwa wa kimiujiza.

“Tulichokifanikisha kama timu bila usaidizi wa tekinolijia ya soka ni kitu kikubwa sana ukizingatia tulicheza na wachezaji tisa kwa kipindi kirefu.

“Ni miujiza. Maamuzi ya refa hayakuwa sahihi. Hii ni historia,” Oktay alisema.