Oktay aanza kuchocha kisa Muivory Coast

Muktasari:

Mastraika hao sasa watang’ang’ania namba na mafowadi wengine wazawa Dennis Oalo, Dickson Ambundo, Nicholas Kipkurui na Dennis Oliech ambaye licha ya ukongwe wake kocha Oktay kasema bado anamhitaji sana.

KOCHA wa Gor Mahia, Hassan Oktay kaanza kuchocha straika wake mpya aliyemshusha kutoka Ivory Coast, atampachikia angalau mabao 25 kwenye msimu wake wa kwanza wa 2019/20.
Baada ya kumnasa straika Francis Afriyie mkutoka Ghana, Oktay alishusha mwingine Gisleun Yikpe Gnamian kutoka Ivory Coast.
Huyu Gnamian, Oktay kamtaja kuwa na uwezo wa kuziba kisawasawa pengo lililoachwa na Jaques Tuyisenge aliyejiunga na Petro Atletico ya Angola.
“Ni straika mzuri sana mwenye ufundi wa kufunga magoli. Nishamcheki mazoezini toka alipowasilia na hakika atasumbua sana nyie subirini. Nimezicheki pia video zake kule alikokuwa na ndio sababu naona akipachika angalau mabao 25 msimu wake wa kwanza. Yaani ukajua nilivyo na hamu kubwa ya msimu uanze ili nimwone akifanya mambo yake, we acha tu,” Oktay kachocha.
Kulingana na Migne, Gnaimian ni mchanga akiwa na miaka 23. Lakini kikubwa kinachomzuzua naye ni kasi yake kubwa aliyonayo pamoja na chenga za maudhi anazosema zitamsaidia sana kuwatoka mabeki wapinzani.
Mastraika hao sasa watang’ang’ania namba na mafowadi wengine wazawa Dennis Oalo, Dickson Ambundo, Nicholas Kipkurui na Dennis Oliech ambaye licha ya ukongwe wake kocha Oktay kasema bado anamhitaji sana.
“Bado tunamhitaji Oliech kwa ajili ya msimu huu mpya na ni jambo analolifahamu pia. Tayari nimeshamjumulisha kwenye listi ya wachezaji nitakaowatumia kwenye dimba la CAF Champions League, hivyo hii ni kuonyesha kuwa  bado nitamhitaji,” Oktay kasema.
Kauli yake OKtay imelenga kuzima tetesi kuwa hamwitaji tena Oliech mwenye miaka 33 na ndio sababu yake ya kufanya usajili mkubwa wa mafowadi kutoka nje na ndani ya nchi.