Ofa ya Barca kwa Neymar noma aisee!

Wednesday June 19 2019

 

BARCELONA, HISPANIA.MAISHA yanakwenda kasi sana asikwambie mtu. Barcelona kwa sasa wanamteka tena Neymar, lakini safari hii huduma yake itawagharimu Pauni 89 milioni pamoja na wachezaji watatu, Samuel Umtiti, Ousmane Dembele na Ivan Rakitic.
Mpango huo wa Barcelona kutaka kutoa pesa pamoja na wachezaji hao watatu ili kupata huduma ya Mbrazili huyo unakuja baada ya rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi kusema mambo hadharani akimshambuliaji staa huyo waliyemnasa kwa Pauni 198 milioni kwamba hakuna aliyemlazimisha kujiunga na timu yao.
Neymar ameshambuliwa vikali kutokana na mambo yake ya kujiunga kwamba amekuwa staa mkubwa kuliko timu, huku akidaiwa kutibuana na wachezaji wenzake akiwamo Kylian Mbappe.
GloboEsporte la Brazil limeripoti kwamba PSG inakaribia kabisa kufanya biashara hiyo ya kuachana na Neymar arudi zake Barcelona, huku wao wakipata pesa na wachezaji watatu, Wafaransa wawili Umtiti na Dembele na kiungo fundi wa mpira kutoka Croatia, Rakitic.
Rais wa PSG, Al-Khelaifi alisema: "Nataka wachezaji ambao watajitolea kila kitu kwa heshima ya jezi ya timu na mipango ya klabu. Wale ambao hawataki au hawaelewi, tutaonana na kuzungumza hilo. Sawa kuna mikataba inapaswa kuheshimika, lakini jambo la msingi kwa sasa kila mtu afuate mipango ya timu."
Neymar amehusishwa pia na Real Madrid, lakini Barcelona wanataka kuwapiga kikumbo wapinzani wao kutokana na kuweka mezani ofa matata.
Real Madrid nao wanataka kumweka kwenye ofa yao Casemiro ili kuwashawishi PSG kuwauzia Neymar ambapo wataweka na mzigo wa pesa mezani.
Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amepanga kukijenga upya kikosi chake ambapo baada ya kunasa mastaa kadhaa akiwamo Eden Hazard sasa anamsaka Paul Pogba na Neymar ili kupafannya Bernabeu kuwa mahali hatari kwa timu pinzani.

Advertisement