Obrey Chirwa kama zali mwanangu!

Muktasari:

Mpaka sasa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi,  jumla ya mabao 20,  yameshatumbukizwa kimiani, huku Chirwa akiwa kileleni akifuatiwa na Kagere na kisha utitiri wa wachezaji waliofunga bao mojamoja, wakati Simba ikiwa pekee hadi sasa kutinga nusu fainali.

UKISIKIA zali ndiyo hili buana, kwani Mzambia Obrey Chirwa anayekipiga Azam FC ashindwe yeye tu sasa kunyakua Tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019.
Straika huyo matata ameonyesha dhamira yake ya kunyakua tuzo hiyo baada ya jioni hii kutupia bao la ushindi kwa timu yake iliyoifunga KVZ mabao 2-1 na kuitupia virago kwenye michuano hiyo.
Chirwa akifunga bao hilo ambalo ni la tatu kwake mpaka sasa katika michuano hiyo katika dakika za lala salama baada ya awali Donald Ngoma kuisawazishia Azam iliyoduwazwa dakika ya 16 na KVZ kupitia kwa Amour Bakar Ali.
Kwa kufikisha mabao matatu kumemfanya Chirwa amwache Mnyarwanda Meddie Kagere mwenye mabao mawili aliyekuwa wanalingana. Kagere jana Jumapili usiku alishindwa kucheza mechi ya Simba dhidi ya KMKM kwa kile kilichoelezwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu.
Hata hivyo, Kagere asubuhi ya leo Jumatatu alifanya mazoezi na wenzake, ila kuna uwezekano mdogo wa kucheza tena kwenye michuano hiyo kutokana na timu yake kuwa na mechi za kimataifa za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kukosekana kwa Kagere na kitendo cha Yanga kutolituma jeshi lake kamili katika michuano hiyo kunatoa nafasi kwa Chirwa kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa Mapinduzi msimu huu, akisahihisha gundu alilokuwa nalo msimu uliopita akiwa na Yanga.
Chirwa akitoka kwao Zambia alicheza mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo na kukosa mkwaju wa penalti ulioing'oa timu yake kwenye michuano hiyo na kusababisha ambebeshe lawama aliyekuwa kocha wake George Lwandamina ambaye alimpanga wakati akijua hakuwa na mazoezi kwani alikuwa kwao akimuuguza mama yake.
Mpaka sasa katika michuano hiyo, jumla ya mabao 20,  yameshatumbukizwa kimiani, huku Chirwa akiwa kileleni akifuatiwa na Kagere na kisha utitiri wa wachezaji waliofunga bao mojamoja, wakati Simba ikiwa pekee hadi sasa kutinga nusu fainali.
Azam iliyopo Kundi B kwa ushindi wa leo, imejiweka katika nafasi nzuri ya kuifuata Simba kwani imefikisha alama 7 ambazo zinaweza kufikiwa na Malindi, Jamhuri na Yanga ambayo usiku huu itavaana na Malindi katika mchezo mwingine wa kundi hilo.

ORODHA YA WAFUNGAJI:
3 Obrey Chirwa (Azam)
2 Meddie Kagere (Simba)
1  Abdulhamid Adam (Mlandege)
   Tafadzwa Kutinyu (Azam)
   Abdul Ramadhani (Jamhuri)
   Shaaban Mohammed (Yanga)
   Abdulswamad Ali (Malindi)
   Juma Hamada (Malindi)
   Evidence Kilongozi (Chipukizi)
   Nichoals Gyan (Simba)
   John Bocco (Simba)
   Mohammed Abdalla (Mlandege)
   Ibrahim Khatib (KMKM)
   Enock Atta Agyei (Azam)
   Haji Mwambe (Jamhuri)
   Donald Ngoma (Azam)
   Amour Bakar Ali (KVZ)