OBFT yawapa mchongo mabondia

Muktasari:

Baada ya mashindano hayo, OBFT itafanya mashindano mengine ya kitaifa mkoani Manyara baadae mwaka huu lengo likiwa kuibua vipaji vya kutosha kabla ya mchujo ili kuunda timu ya taifa ambayo itaanza mazoezi kujiandaa na mashindano ya kimatifa.

SHIRIKISHO la Ngumi za wazi (OBFT) limewapa mchongo mabondia kwa kuwaita wenye sifa kushiriki mashindano ya wazi ya taifa yatakayoanza kesho Jumatatu Agosti 3, 2020 jijini Dar es Salaam.

Rais wa OBFT, Mutta Lwakatare amesema mashindano hayo ni mwanzo wa maandalizi ya kuunda timu ya taifa itakayoandaliwa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ikiwamo michezo ya Olimpiki mwakani.

Lwakatare amesema mikoa ya Njombe, Iringa, Mwanza, Morogoro, Pwani Singida, Mbeya na wenyeji Dar es Salaam, imethibitisha kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Parkers, Kawe.

Pia timu za taasisi za Majeshi ya ulinzi na usalama pia zitashiriki katika mashindano hayo yatakayofanyika kwa siku saba.

Amesema msimu huu mashindano hayo ni ya wazi na bondia yoyote mwenye sifa anaruhusiwa kushiriki, kwani wanahitaji kuibua vipaji vipya vya ndondi za ridhaa, hivyo bondia yoyote hata kama hana klabu, lakini ana sifa atapewa nafasi ya kuonyesha uwezo wake.

"Mabondia waje kwa wingi, kwani mwakani kila mmoja anafahamu kuna mashindano makubwa ya Olimpiki, hivyo maandalizi yanatakiwa kuanza mapema kwa kupata timu itakayokuwa na imejiandaa vyema ndio maana tumeweka uhuru kwa wanamasumbwi wote kujitokeza.

Amesema mabondia wa ngumi za kulipwa pia wanaruhusiwa kujitokeza kushiriki lakini kwa utaratibu uliowekwa wa kuandika barua.

"Jumatatu asubuhi tutakuwa na zoezi la upimaji uzito na afya kwa mabondia kabla ya kuanza mashindano baadae mchana," amesema.