Nyuma ya pazia kiwango cha De Gea kwa Spurs

Muktasari:

  • Mechi hiyo ilimalizika kwa kikosi chake cha Man United kushinda 1-0, shukrani kwa bao la Marcus Rashford, lakini kama isingekuwa kiwango matata cha kipa De Gea, basi hii leo, stori zingekuwa tofauti kabisa.

LONDON, ENGLAND .SIKIA, nakunong’oneza. Usimwambie mtu, David De Gea anatafuta mkataba mpya Manchester United.

Miezi michache iliyopita, hasa kule kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2018, kipa hiyo Mhispaniola alionekana kuwa wa kawaida sana.

Wadau wa mambo wanasema kwamba ingekuwa ngumu kuwashawishi Man United kumlipa mshahara mkubwa kwenye dili mpya kama si kwa kile alichokifanya Jumapili iliyopita uwanjani Wembley.

Kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Hotspur, yenye washambuliaji wenye shabaha kwenye kufunga kama Harry Kane, kipa De Gea aliokoa hatari 11 na kuondoka uwanjani hapo salama kabisa bila ya kuokosa mpira hata mara moja kwenye wavu wake.

Mechi hiyo ilimalizika kwa kikosi chake cha Man United kushinda 1-0, shukrani kwa bao la Marcus Rashford, lakini kama isingekuwa kiwango matata cha kipa De Gea, basi hii leo, stori zingekuwa tofauti kabisa.

Kiwango chake kwenye mechi hiyo kilisifiwa na kila mtu, wakiwamo wachezaji wenzake wa Man United na sasa, De Gea anawasubiria mezani mabosi wa timu hiyo kumpelekea mkataba safi utakaomfanya aweke kibindoni Pauni 300,000 kila wiki kama mshahara wake.

Lakini, je, kiwango hicho cha De Gea kimemfanya kuwa kipa matata zaidi kwenye Ligi Kuu England kwa maana ya kuokoa hatari nyingi kwenye mechi moja kuliko yeyote?

Sikia sasa. Kiwango kile cha De Gea, ambaye aliwahi kuidakia pia Atletico Madrid, kinamfanya ashike namba tatu kwenye kipindi cha miaka 15 kwa makipa waliokoa hatari nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England, kwa mujibu wa utafiti wa Your-Promotional-Code.co.uk.

Kipa, Tim Krul ndiye anayeshikilia rekodi ya kuokoa hatari nyingi zaidi kwenye mechi moja ya Ligi Kuu England, wakati alipookoa mara 14 kwenye mechi dhidi ya Tottenham pia, mwaka 2013.

Kisha anakuja, Mdachi Edwin van der Sar, ambaye aliokoa hatari 12 kipindi hicho akiwa Fulham kwenye mechi dhidi ya kikosi kile cha Arsenal isiyofungika, mwaka 2003.

Lakini, kwa makipa waliopo sasa kwenye Ligi Kuu England, hakuna anayemzidi De Gea kwa kuokoa hatari nyingi kwenye mechi moja.

Kiwango chake kwenye mechi hiyo ya Jumapili, hakika De Gea alikuwa kwenye ubora wake, akiokoa hadi kwa kutumia miguu, kama lile shuti la hapo kwa hapo la Kane.

Kilikuwa kiwango bora pia kwa Mhispaniola huyo katika maisha yake yote ya soka.

Kwa kifupi tu, De Gea hakuwa amewahi kuokoa hatari zinazozidi tarakimu mbili kwenye mechi moja hadi hapo alipofanya hivyo mara 11 kwenye mchezo huo wa Jumapili iliyopita.

Huko nyuma alishawahi kuokoa hatari tisa, ilikuwa dhidi ya Tottenham katika msimu wa 2011-12 na hatari nane aliokoa kwenye mechi nne tofauti.

Kwenye mechi hizo nne, ambazo De Gea aliokoa hatari nane nane, alifanya hivyo dhidi ya Liverpool na Everton kwenye Ligi Kuu England na huko alikotoka kwenye La Liga, alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Getafe na Gijon.

De Gea aliwahi pia kuokoa hatari saba kwenye mechi tatu tofauti, dhidi ya Crystal Palace, Bournemouth na Mallorca.

Kuhusu ushujaa wa De Gea huko Wembley, msemaji wa Your-Promotional-Code.co.uk alisema: “Si jambo la kawaida kwa klabu kubwa kumruhusu mpinzani kupiga mashuti mengi yanayolenga goli kwenye mechi moja kwa namna ile.

“Sawa hakuna ubishi kwamba David de Gea ni moja ya makipa bora kabisa duniani, lakini kila kiwango chake dhidi ya Tottenham kimeonyesha tu umuhimu wake kwenye kikosi cha Man United United.

“Akiwa na umri wa miaka 28, unachotarajia kwake ni kumwona akipevuka zaidi kama mchezaji na hakika Manchester United matumaini yao atabaki kwenye kikosi chao kwa ajili ya usalama wao.”