Nyuma ya pazia gemu ya Man United, Liverpool

Muktasari:

Liverpool wanavaa jezi nyekundu? Basi James Milner bana amesema alipokuwa mdogo baba yake alimpiga marufuku kabisa kuvaa nguo yoyote yenye rangi nyekundu.

ILE siku ndio kesho Jumapili. Manchester United itacheza na Liverpool huko Old Trafford. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amekiri Ole Gunnar Solskjaer si Jose Mourinho, hivyo inawatarajia Man United tofauti kabisa hiyo kesho. Solskjaer hajapoteza mechi kwenye ligi tangu alipoanza kuinoa timu hiyo.

Klopp aliichapa Man United kwenye mechi ya kwanza ya ligi, 3-1 na hapo ikawa mwisho wa Mourinho kuinoa timu hiyo.

Akafutwa kazi na Ole amekuja kubadili upepo. Man United kwa sasa haikamatiki na hilo linamtisha Klopp katika mbio zake za kusaka ubingwa.

Man United na Liverpool zinapokutana, hazijawahi kuwa kitu cha kawaida.

Wakongwe kibao wa Man United akiwamo Rio Ferdinand na Mikael Silvestre walikwenda kwenye mazoezi ya timu hiyo, ikielezwa kwenda kumpa mzuko Ole ili awachape Liverpool hiyo kesho Jumapili. Upinzani wa Man United na Liverpool ndio unaomfanya staa wa huko Anfield, Mwingereza James Milner kufichua kitu.

Si unajua Liverpool wanavaa jezi nyekundu? Basi James Milner bana amesema alipokuwa mdogo baba yake alimpiga marufuku kabisa kuvaa nguo yoyote yenye rangi nyekundu.

Lakini, sababu ya marufuku hiyo mashabiki wa Liverpool itaifurahia. Ilikuwa Man United.