Nyuma ya mechi 250 za Klopp Liverpool

Muktasari:

Hizi hapa data zilizopo nyuma ya mechi 250 za mwanzo za Klopp kwenye kikosi hicho cha Liverpool tangu alipobeba mikoba ya kukinoa kikosi hicho Anfield miaka mitano iliyopita.

LIVERPOOL ,ENGLAND . LIVERPOOL mwaka wake huu. Pengo la pointi 22 kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na mambo yamekuwa matamu pia kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako ipo kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora.

Lakini, Jumanne iliyopita ilichapwa bao 1-0 na Atletico Madrid katika mchezo wa kwanza wa raundi hiyo uliofanyika uwanjani Wanda Metropolitano.

Kwenye Ligi Kuu England, mchezo wake wa mwisho kucheza ni ule uliokuwa wa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Norwich City, ambapo hiyo ilikuwa mechi ya 250 tangu kikosi hicho kilipoanza kuwa chini ya Kocha Mjerumani, Jurgen Klopp.

Hivi unavyosoma hapa ina maana Klopp ameiongoza Liverpool katika mechi 251. Mjerumani huyo tangu alipotua Anfield, Oktoba 2015, ameibadili Liverpool kuwa timu ya kibabe ikinyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Klabu Bingwa Dunia na sasa inaelekea kubeba taji la Ligi Kuu England baada ya kusubiri kwa miaka 30.

Hizi hapa data zilizopo nyuma ya mechi 250 za mwanzo za Klopp kwenye kikosi hicho cha Liverpool tangu alipobeba mikoba ya kukinoa kikosi hicho Anfield miaka mitano iliyopita.

– Katika mechi hizo 250 klabuni Liverpool, Klopp ameshinda 153, sare 58 na vichapo 39, akiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 61.2.

– Ndani ya mechi hizo, Liverpool imefunga mabao 539 na kufungwa mabao 261.

– Klopp ushindi wake wa mechi 153 katika mechi 250 za kwanza hiyo imemfanya awafunike makocha wengine kina Kenny Dalglish aliyeshinda mechi 152 na Bob Paisley mechi 140.

– Katika mechi hizo, Klopp ameifikisha Liverpool kwenye fainali sita akipoteza tatu za mwanzo (Kombe la Ligi, Europa League na Ligi ya Mabingwa Ulaya) na kushinda tatu zilizofuatia (Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup na Klabu Bingwa Dunia).

– Ndani ya idadi hiyo ya mechi, Klopp ametumia wachezaji 84 tofauti katika michuano yote aliyoiongoza Liverpool.

– Roberto Firmino ndiye mchezaji aliyetumika mara nyingi zaidi na Klopp, akicheza mechi 221 za michuano yote chini ya kocha huyo Mjerumani. Firmino anafuatiwa na James Milner, mechi 196 na Georginio Wijnaldum mechi 171.

– Straika Mohamed Salah ndiye staa aliyefunga mabao mengi zaidi chini ya Klopp, akifanya hivyo mara 89. Wanaofuatia ni Firmino (mabao 76) na Sadio Mane (mabao 74) kwenye tatu bora yake.

– Kwa mujibu wa Transfermarkt, ambao data zao za asisti zinadaiwa hazina usahihi sana, Firmino ndiye mchezaji aliyepiga asisti nyingi chini ya Klopp akifanya hivyo mara 59, akifuatiwa na Salah (41) na Milner (38).

– Klopp amesajili wachezaji 14 wa kikosi cha kwanza ndani ya miaka yake mitano hapo Anfield kwa gharama ya pamoja ya Pauni 403.5 milioni, sawa na wastani wa Pauni 28.8 milioni kwa kila mchezaji.

– Beki wa kati Virgil van Dijk ndiye mchezaji wa bei mbaya zaidi aliyemsajili Klopp kwa Pauni 75 milioni, wakati beki mwingine Ragnar Klavan ndiye mchezaji aliyemsajili kwa pesa ndogo zaidi, Pauni 4.2 milioni.