Nyuki wasimamisha mechi ya Yanga, Gwambina

WADUDU aina ya nyuki walisimamisha mpira wa Gwambina dhidi ya Yanga kwa takribani dakika moja baada ya kukatiza katikati ya Uwanja wa Gwambina.

Nyuki hao walikatiza wakati kipindi cha pili kilipokuwa kinaanza hali iliyowafanya wachezaji wote walale chini ya uwanja.

Wakati wachezaji hao wakiwa wamelala chini, mashabiki nao waliokuwa uwanjani hapo walionekana kila mmoja akihangaika kupata namna ya kujikinga na nyuki hao.

Hata hivyo hawakukaa muda mrefu wakaondoka na mpira kuendelea kipindi cha pili.

Licha ya mashambulizi yaliyofanywa na timu zote, lakini hadi mapumziko siyo Gwambina wala Yanga aliyeweza kuona lango la mwenzake.

Pamoja na kupumzika kwa nguvu sawa ya bila kufungana, Yanga itajilaumu zaidi kutokana na nafasi walizopata zaidi ya moja lakini papara na kutotulia kwa straika wake ndio iliwapa matokeo hayo.

Gwambina walicheza kwa umakini haswa kwa kujilinda sana, huku wakishambulia kwa kushtukiza na kutengeneza nafasi kadhaa japokuwa umaliziaji pia ulikuwa butu.

Bado Waziri Junior hajaweza kutakata kwani mipira aliyopewa na Tuisila Kisinda ilimpita pembeni, huku eneo la katikati likiongozwa na Abdulazizi Makame pia lilipotea na zaidi beki nayo haikuwa sawa kwa Yanga.

Pamoja na Gwambina kucheza kwa kujilinda sana, lakini walifanya shambulizi ambalo liliipa bao kupitia kwa Nahodha wake, Jacob Masawe dakika ya 34 licha ya mwamuzi Abdulazizi Ally (Arusha) kuonesha mfungaji kuotea.

Yanga waliendelea kushambulia ambapo dakika ya 38 Tuisila Kisinda akiwa na Mpira alikosa utulivu na kupiga shuti kali ambalo halikuwa na madhara langoni mwa wapinzani na kuishia mikononi mwa Kipa Ibrahim Isihaka.

Hadi dakika 45 za awali zinamalizika, mwamuzi Hussein Athuman kutoka Katavi alimuonesha kadi ya njano, Salum Kipaga baada ya kumchezea rafu Kisinda dakika ya 36 ikiwa ni kadi pekee iliuotolewa tu.