Nyuki wasimamisha mchezo wa netiboli

Muktasari:


Mchezo ulilazimika kusimama kwa dakika kadhaa ili kuwaondoa nyuki hao, lakini baadaye vurumai lilizuka kwa JKT Makutupora kudai kubaniwa dakika mbili

MASHINDANO ya Klabu Bingwa Taifa yanafikia tamati Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini hapa ambapo bingwa wa ligi hiyo atajulikana baada ya kumalizika kwa mechi zote zilizoshirikisha timu 10.
Lakini, ligi hiyo ikitarajiwa kumalizika, wadau watabaki na kumbukumbu ya tukio la nyuki kuvamia nguzo ya goli wakati wa mchezo kati ya Tamisemi na JKT Makutupora.
Ni mchezo huo uliosababisha sintofahamu baada ya mchezo kumalizikia gizani ili kukamilisha muda sahihi wa mchezo katika robo ya nne, ambapo timu ya JKT Makutupora hawakukubaliana na filimbi ya waamuzi kumaliza mchezo.
Tukio zima lilianzia kwenye robo ya kwanza kati ya nne pale nyuki walipotokea kusikojulikana na kutua kwenye goli la kaskazini mwa uwanja huo na kuingia ndani ya chuma na nyavu za goli hilo na kusababisha taharuki kwa wachezaji na mashabiki.
Baadhi ya wachezaji na mashabiki walilazimika kukimbia uwanja huku jitihada za kuwaondoa kwa kupuliza dawa zikiendelea.
Baadaye mambo yaliwekwa sawa huku muda ukiwa umekwenda lakini, waamuzi walilazimika kuendelea licha ya giza kuingia na mchezo ukiwa umebakiza robo ya mwisho.
Kikao cha dharura kikafanyika na makubaliana yakawa mchezo kuendelea ili kukamilisha robo ya mwisho wakati huo Tamisemi wakiongoza kwa pointi 34 dhidi ya 27 za JKT Makutupora. Hata hivyo, katika sintofahamu waamuzi wakapuliza filimbi kuashiria mchezo umemalizika na hapo ndipo JKT Makutupora wakalianzisha kwa kuwazonga waamuzi wakidai zimebaki dakika mbili hivyo lazima zimalizike.
Vurumai hilo lililoshuhudiwa na Mkurugenzi wa Michezo Yusuph Singo, lilitulizwa na Katibu wa Chama cha Netiboli Taifa, Judith Ilunda ambaye aliwatuliza viongozi wa JKT waliokuwa na hasira wakiamini wameonewa.
Kuhusu hatma ya mchezo huo, Ilunda alilieleza Mwanaspoti kuwa: “Mchezo umekamilika kwa dakika zote na matokeo yanabaki kama yalivyo na kila kitu kitaendelea kama kilivyopangwa”.