Nyota wanne kwa mpigo wanukia Mbao FC

Wednesday July 11 2018

 

By Saddam Sadick

Mbao  FC inaendelea kufanya mambo yake kimyakimya na muda wowote inatarajia kuwasainisha wachezaji wanne kwa mpigo kutoka timu tofauti ikiwa ni kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu.
Timu hiyo ya jijini Mwanza, tayari imeshaondokewa na nyota wake watatu ikiwa ni aliyekuwa Nahodha, Yusuph Ndikumana aliyejiunga na KMC, Habib Kyombo na Boniface Maganga waliotimkia na Singida United.
Habari ilizonasa gazeti hili ni kwamba wachezaji, Peter Mwangosi (Njombe Mji), Zamu Kufo (African Lyon), Andrea Kiape (JKU) na Emanuel Mfumbuka wa Dodoma FC tayari wapo jijini Mwanza wakisubiri kumalizana na uongozi ili kuanza kazi.
“Wapo wachezaji wanne ambao wamesubiri maelekezo ya mwisho ili kuanza kazi na ukizingatia muda ni mchache, lakini si hao tu bali uongozi unaendelea kuwasiliana na nyota wengine ili kujiunga na timu,” kilisema chanzo hicho.
Kocha wa Klabu hiyo, Amri Said ‘Stam’alisema kuwa kwa sasa wanaendelea vyema na mazoezi na kwamba kikubwa anavutiwa na kiwango cha vijana wake na jinsi wanavyomuelewa.
Alisema kuwa hadi sasa wachezaji takribani wa kikosi cha kwanza wameshawasili kambini wakiendelea kujifua na kusema kuwa hataki kupoteza muda kwani ratiba imebana.

Advertisement