Nyota wa kikapu Mwanza apata shavu nchini Canada

Muktasari:

Ally ambaye alishiriki vyema Michuano ya Kanda 5 kwa nchi za Afrika yaliyomalizika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam na kuwa miongoni mwa wachezaji watano bora,anatarajia kuondoka kesho Jumapili nchini kuanza safari ya maisha huko Canada.

NYOTA ya mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana (U-18) ya mchezo wa Kikapu,Atiki Ally  imeendelea kung’ara baada ya kupata shavu kwenda nchini Canada kwa ajili ya masomo pamoja na kuendeleza kipaji chake katika mchezo huo.

Akizungumza na Mwanaspoti,nyota huyo alisema kuwa matarajio yake ni kufanya vizuri huko nje ya nchi kwa kuzingatia kile atakachoelekezwa ili kuweza kufikia ndoto zake za kuwa mchezaji Bora bora wa Kikapu na kuitangaza vyema Tanzania.

“Ninaamini nitafanya vizuri kutokana na kipaji changu hii ni fursa nzuri ambayo sipaswi kuichezea,nitakuwa makini kufuata kile ninachofundishwa ili kufikia malengo yangu ya kuwa mchezaji Bora wa Kikapu ulimwenguni”alisema Ally.

Kwa upande wake Kocha Bahati Mgunda,alisema kuwa uwezo na kipaji cha mchezaji huyo huenda akawashangaza wengi kwenye ulimwengu wa mchezo wa Kikapu kutokana na uwezo na kipaji alichonacho.

“Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo na kipaji binafsi na isitoshe umri wake bado mdogo kwahiyo huenda akafanya vizuri zaidi na kuitangaza vyema Tanzania katika mchezo wa Kikapu duniani”alisema Mgunda.

Naye Mama mzazi wa mchezaji huyo,Hadija Abdul alisema kuwa licha ya kupitia changamoto nyingi haswa kuhangaika kutafuta vifaa vya michezo kutokana mguu mkubwa wa mwanaye huyo lakini kwa sasa anaona fahari kwa fursa hiyo aliyopata.

“Ni furaha kubwa sana kuona mtoto wangu anaenda kusomeshwa bure na kuendelezwa kipaji chake nje ya nchi,tumepitia changamoto nyingi haswa kuhangaika na vifaa vya michezo kutokana na kuwa na mguu mkubwa”alisema Abdul.

Mwisho….