Nyota wa Southampton aikana England, Nigeria

Muktasari:

Hatimaye mshambuliaji chipukizi wa timu Southampton, Michael Obafemi, 18, amekata mzizi wa fitina kwa kuamua kucheza katika timu ya Taifa la Jamhuri ya Ireland badala ya nchi yake ya asili Nigeria na England alikokulia ambako alikuwa akihitajiwa.

London, England. Mshambuliaji chipukizi wa Southampton, Michael Obafemi, 18, amechagua kulitumikia Taifa la Jamhuri ya Ireland na kuziachia mshangao Nigeria na England.

Obafemi alizaliwa mjini Dublin, Ireland na kukulia jijini London, lakini wazazi wake wakiwa na asili ya Nigeira ambao walikwenda Ireland kwa ajili ya kutafuta maisha na mchezaji huyo alikuwa na fursa ya kuchagua nchi yoyote kati ya hizo.

Tayari alicheza katika timu za vijana za Taifa za England kabla ya kocha Martin O'Neill kumuita katika kikosi cha vijana chini ya miaka 19 cha Ireland, siku chache baada ya kocha wa timu ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ Gernot Rohr, kumuita kwenye kikosi chake.

Mchezaji huyo alikubali wito wa Ireland lakini Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa) likaionya nchi hiyo kumtumia katika mechi moja pekee badala ya mbili zilizokuwa zikiwakabili kwa kuwa kikanuni akicheza mechi zote Shirikisho hilo litamuidhinisha rasmi kuitumikia.

Hata hivyo kabla ya kucheza mechi hizo mchezaji huyo baada ya mazungumzo yaliyohusisha familia yake na viongozi wa Chama cha soka Ireland ameichagua nchi hiyo kuitumikia katika maisha yake yote ya kisoka.

Kanuni za Fifa zinamruhusu mchezaji ambaye ataichezea nchi moja katika timu za vijana chini ya miaka 23 ambaye kutokana na sababu za nasaba au kuhama Taifa kubadilisha uamuzi na kuichagua nchi nyingine ikiwa bado hajaitumikia timu ya wakubwa ya Taifa la awali.

Kocha O'Neill alimpanga mchezaji huyo katika ya kirafiki dhidi ya Ireland Kaskazini uliochezwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Aviva Stadium na O'Neill alisema hatamtumia katika mchezo dhidi ya Denmark utakaochezwa leo wa Nations Ligi.