Nyota wa Simba awatuliza mashabiki Biashara Utd

Wednesday October 10 2018

 

By SADDAM SADICK

STRAIKA wa Biashara United,Uhuru Suleiman ambaye amewahi kuitumikia klabu ya Simba, ameangalia mwenendo wa timu yao katika Ligi Kuu na kusema kuwa ugeni kwa viongozi na wachezaji katika michuano hiyo ndio inawatesa kwa sasa na kuwatoa hofu mashabiki kuwa mambo yatakaa sawa.

Biashara United ya mkoani Mara ndio mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu msimu huu,ambapo kati ya mechi nane walizocheza hivi sasa imekusanya pointi tisa na kukaa nafasi ya 15 kwenye msimamo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu jijini Mwanza,Suleiman alisema kuwa kwa sasa timu hiyo inatatizwa na ugeni kwa viongozi na wachezaji ambao wengi wao ndio mara ya kwanza kushiriki Ligi Kuu.

Alisema kuwa kikubwa ni mashabiki kutulia na kuipa muda timu yao kwani kwa kiwango walichonacho wachezaji ndani ya uwanja watafanya kweli na kuweza kumaliza Ligi katika nafasi nzuri.

“Bado timu ni changa kwenye Ligi Kuu,iwe kwa wachezaji na hata viongozi kwahiyo ni suala ya kuipa muda ili kuzoea,niwaombe mashabiki watulie na kuisapoti tutafanya vizuri”alisema Suleiman.

Nyota huyo wa zamani wa Klabu za Simba na Lipuli alisema kuwa licha ya kwamba hajabahatika kufunga bao lakini kiwango chake kimeongezeka tofauti na alivyokuwa miaka ya nyuma.

Mshambuliaji huyo alikiri kuwa Ligi ni ngumu lakini mpira ni ule ule na kwamba anayepata nafasi na bahati ya matokeo ndiye anashinda na kwamba Biashara muda wake utafika na watashangaza wengi.

“Kwa ujumla timu ni nzuri hata mazoezi tunayoyafanya chini ya Kocha wetu (Hitimana Thiery) ni mazuri lakini pia kiwango changu naona kimepanda sana kulinganisha na miaka iliyopita”alisema Straika huyo.

 

 

Advertisement