Nyota tegemeo kung’oka Liverpool

Muktasari:

  • Liverpool ilikuwa ikikimbiza ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kasi, lakini Jumapili iliyopita walikatwa maini na Manchester City baada ya kambi ya Etihad kuibuka kidedea

 

Nyota tegemeo wa Liverpool, Virgil van Dijk anaweza kuondoka katika klabu hiyo kama wakishindwa kupata ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Liverpool ilikuwa ikikimbiza ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kasi, lakini Jumapili iliyopita walikatwa maini na Manchester City baada ya kambi ya Etihad kuibuka kidedea, sasa akili zote za viongozi na wachezaji wa Liverpool zimehamia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na watacheza fainali na Tottenham.

  Virgil van Dijk amekuwa akicheza kwa kiwango tangu alipohamia katika klabu hiyo akitokea Southampton kwa ada ya Pauni 75 milioni mwaka 2018. Lengo lake kubwa ni vikombe na kama hakupata, kuna dalili kubwa akaondoka. Mtu mmoja wa karibu na mchezaji huyo alisema nyota huyo atahama dirisha kubwa la usajili linalokuja kama ndoto yake haitatimia.

"Sidhani kama ataendelea kuwepo baada ya fainali za Ligi ya Mabingwa, yeye ni mtu mwenye njaa ya vikombe. Akikosa katika timu yake ya sasa atakwenda kutafuta katika timu nyingine,"alisema mtu huyo.

Mchezaji huyo alipewa taji la mchezaji bora wa Mwaka wa EPL wiki iliyopita kutokana na juhudi kubwa aliyoonyesha msimu mzima.