Nyota kikapu Taifa wagoma kisa maandalizi

Muktasari:

Ingawa Rais wa TBF, Phares Magesa amekanusha akisema changamoto binafsi zilikwamisha wachezaji hao kutoambatana na timu, Baraka amesema utaratibu wa safari ya timu ya taifa uliwabagua baadhi ya wachezaji.

Wakati jana Jumatano Tanzania ikitupa kete yake ya kwanza kwenye mashindano ya kanda ya kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za kikapu kwa mataifa ya Afrika za 2021, nyota 10 kati ya 17 wameitosa timu ya taifa.

Tanzania iliyoondoka na wachezaji saba pekee huku baadhi ya nafasi zikiwa na mchezaji mmoja mmoja ilicheza mechi ya kwanza na Kenya kwenye Uwanja wa Nyayo jana jioni.

Awali, Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) liliwaita nyota 17 wakiwamo wa kimataifa waliokuwa wakijifua kwenye Uwanja wa Ndani ya Taifa kujiandaa na mashindano hayo na 10 kati yao kutoambatana na timu katika dakika za mwishoni.

Baadhi ya wachezaji akiwamo aliyekuwa nahodha wa Timu ya Taifa, Baraka Athumani walisema, shirikisho na benchi la ufundi hawakutaka wasafiri na timu kwa makusudi.

Ingawa Rais wa TBF, Phares Magesa amekanusha akisema changamoto binafsi zilikwamisha wachezaji hao kutoambatana na timu, Baraka amesema utaratibu wa safari ya timu ya taifa uliwabagua baadhi ya wachezaji.

“Sikupenda tulivyofanyiwa, bora wasingetuita kwenye timu,” alisema Baraka ambaye anashikilia tuzo ya mfungaji bora wa mashindano ya Afrika kanda ya tano msimu huu.

Alidai kocha na TBF waliitisha safari hiyo kienyeji bila kufuata taratibu.

“Wachezaji wa JKT ni watumishi wa Serikali na Kocha wa Timu ya Taifa, Alfred Ngalaliji anafahamu taratibu ili tuweze kusafiri na timu ya taifa tunapaswa kuombewa ruhusa, lakini hakufuata taratibu hizo kwa kigezo kwamba tuko likizo,” alisema Baraka.

Jimmy Brown anayecheza Philippines alisema amejiondoa kutokana na maandalizi hafifu.

Jimmy ambaye alijifua na timu hiyo kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa hadi siku ya mwisho kabla ya safari alisema utaratibu ambao TBF inautumia katika uteuzi wa timu ya taifa na maandalizi ndivyo vimemuondoa kikosini.

Magesa alikiri baadhi ya wachezaji kujiondoa kwenye timu kwa sababu binafsi, lakini wengine hawakuwa na nyaraka muhimu za kusafiria (pasipoti).

“Wachezaji wa JKT wao ni ishu nyingine lakini hiyo sisi haituhusu kwani kocha wa timu ya taifa ndiye kocha wa JKT, hivyo anafahamu taratibu zote,” alisema.

Walioachwa mbali na Baraka na Jimmy wengine ni Musa Chacha, Kaikai Lek, Sudi Ulanga, Enrico Augustino, Cornelius Peter, Amin Mkosa, Fadhili Chuma, Mwalimu Heri, Jackson Brown na Gwalugano John.

“Baadhi yao waliomba udhuru, wengine walikuwa na matatizo ya kifamilia na wengine walitoka kwenye timu kwa sababu binafsi, tuwaombee waliopo Kenya wafanye vizuri,” alisema.

Alisema wachezaji waliosafiri ndiyo wana vigezo kwani ndiyo walikuwa tayari kusafiri na timu hiyo ya taifa.

Wachezaji hao ni Stephano Mshana, Erick John, Ally Mohamed, Cornelius Peter, Ladislaus Lusajo, Issaya Aswile na Haji Mbegu ambao watakata utepe dhidi ya wenyeji Kenya kwenye Uwanja wa Nyayo.