Nyota hawa Derby imewakalia vibaya

Wednesday July 8 2020

 

By Khatimu Naheka

JUMAPILI kutakuwa na pambano kali inawezekana likawa la kufungia msimu, wakati Yanga itakapokutana na Simba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Mchezo huu utaamua nani kati ya timu hizi mbili ambazo ni watani wa jadi itatinga katika fainali wakisubiri mshindi kati ya Sahare All Stars watakaokutana na Namungo FC.

Yanga na Simba siku zote sio mchezo wa masikhara, unaweza ukapeleka furaha timu moja kisha huzuni kwa nyingine, lakini kuna wakati hata unaweza kupoteza ajira ya wachezaji, viongozi na hata makocha endapo matokeo yakiwa mabaya na hawa wanapaswa kuwa makini na mechi hii.

Sven Vandenbroeck (Simba)

Kocha Mkuu wa Simba huyu ataingia katika mchezo huu akiwa ameshatoa sare moja na akapoteza mechi moja. Kifupi ameambulia pointi moja mbele ya Yanga.

Akipoteza mchezo huu wa nusu fainali atakuwa amepoteza mechi ya pili ya watani na hii sio habari nzuri kwake kwani, haitashtua kusikia amepoteza kazi licha ya kwamba amewapa Simba taji la Ligi Kuu Bara msimu huu akiwapa pia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Advertisement

Bernard Morrison (Yanga)

Kwa wiki mbili sasa mshambuliaji huyu wa Yanga, Bernard Morrison amekuwa akivuma katika vyombo vya habari akisumbuana na mabosi zake juu ya mkataba wake, mpasuano huo ukafika hadi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mbele ya kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ili kutafuta ufumbuzi.

Ghafla wiki hii mapema akageuka na kurejea kazini, lakini mbaya zaidi kwake ni kwamba, vurugu zote hizi zimekuwa zikitajwa kuwa Simba wako nyuma yake.

Hakuna shaka kwamba Morrison atacheza mchezo huu, lakini salama yake ni kuomba Yanga ishinde ila ikipoteza au pia ikatokea hakucheza kwa kiwango chake basi anaweza kujikuta kwenye wakati mgumu mbele ya mashabiki. Wanahisi anakwenda Simba hivyo kazi yake ni kufanya kazi ya kuwathibitishia kwa vitendo kwamba, yuko pamoja nao.

Farouk Shikhalo (Yanga)

Kipa raia wa Kenya, kuna uwezekano mkubwa akawa golini Jumapili, hii itakuwa mechi yake ya pili akitangulia kuambulia sare ya mabao 2-2. Akikaa langoni kisha timu yake kupoteza tena makosa yakiwa kwake basi huenda akajikuta kwenye wakati mgumu kutokana na makipa wa Yanga kufungwa mabao ya kizembe katika mechi za karibuni.

Hii ndio mechi ya kufuta makosa ya kizembe na kujiweka vizuri kwani, dirisha la usajili linakaribia.

Aishi Manula (Simba)

Uwezekano wa kipa Aishi Manula kukaa golini ni mkubwa, kuna wakati anakubalika na kuna wakati analaumiwa, dua yake inatakiwa kuwa mechi hii imalizike salama kwa timu yake, ikitokea amepoteza kisha kuonekana amefanya makosa lolote linaweza kutokea kwa kubebeshwa lawama.

Akiteleza kwenye mchezo huu itatoa mwanya mwa wapinzani wake kufukua faili ya Benno Kakolanya, ambaye analalamika kubaniwa na kutupwa jukwaa kama kipa wa tatu.

Pascal Wawa (Simba)

Beki wa Simba huyu raia wa Ivory Coast, bado hatma yake ndani ya timu hiyo haijaeleweka ingawa muda wowote atapewa mkataba mpya wa mwaka mmoja.

Ikitokea amepoteza mechi hii haitashtua kusikia mpango wa mkataba mpya umeota mbawa. Moja ya maeneo ambayo Simba wanapanga kufanyia kazi kwenye usajili mpya ni beki wa kati pale.

David Molinga (Yanga)

Kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga ni David Molinga ‘Falcao’ naye hatofautiani sana na Manula, kuna wakati anakubalika na kuna wakati anakuwa katika nyakati za lawama.

Mechi zote mbili dhidi Simba hakucheza lakini, hii kuna kila dalili akawa uwanjani na salama yake ni Yanga ishinde ila ikitokea akacheza kisha timu yake kupoteza kuna uwezekano safari yake ikaiva na msimu ujao Jangwani wasiwe na Molinga. Hata hivyo, tayari ana dili tamu huko Morocco.

Kelvin Yondani (Yanga)

Beki wa Yanga ambaye mara nyingi mechi kama hizi zimekuwa zikimfanya kuwa shujaa na hata adui. Yondani mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na bado hajapewa taarifa kuhusu mkataba mpya. Kama nahodha wake Papy Tshishimbi atakosekana uwanjani basi kuna uwezekano mkubwa Yondani akacheza mechi hii na ikiwa hivyo, kisha matokeo yakawa tofauti na basi kiwango chake ndio kitatoa majibu.

Hata hivyo, Yondani amekuwa mhimili mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga.

Jonas Mkude (Simba)

Kiungo mkabaji wa Simba amekuwa katika nyakati ngumu ndani ya kikosi hicho hasa timu yake inapopoteza na hata ikishinda huwa hakumbukwi kwa pongezi. Hata kwenye mchezo huo, Mkude anatakiwa kuwa makini nao kwani Simba ikipoteza hakuna shaka katika wachezaji watatu watakaolaumiwa jina lake litakuwa juu ya orodha ya lawama za mashabiki. Maisha yake ndani ya Simba yamekuwa hivyo, na inawezekana hata mwenyewe ameshazoea.

Muharami Issa (Simba)

Kocha wa makipa wa Simba huyu dua yake inatakiwa kuwa timu yake ishinde unajua kwanini?

Muharami analaumiwa kuwa anambeba sana Manula kiasi cha kumuondoa kikosi cha kwanza kipa mwingine Benno Kakolanya. Simba ikifungwa sakata hili la makipa hawa litamletea shida kama sio kumpotezea ajira kocha huyu. Mwamuzi wa haya yote ni dakika 90 za mchezo hapo Jumapili Taifa.

Advertisement