Nyota Yanga wapita mlango wa nyuma

BAADHI ya wachezaji wa Yanga, wameamua kutokea mlango wa nyuma baada ya kumalizana na uongozi wao.

Yanga imefanya kikao kizito na wachezaji wao leo Jumatatu Agosti 03, 2020, kinachoamua hatma yao ya kubaki ama kuachwa msimu ujao, kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam.

Mashabiki wakiwa wanawasubiri wachezaji hao, katika mlango mkubwa Andrew Vicent 'Dante', Raphael Daudi, Said Mussa, Tariq Seif na Paul Godfrey ndio waliopita mlango wa nyuma na kutokomea.

Ukiachana na hao, nahodha wa timu hiyo, Papy Tshishimbi ambaye kumekuwa na sintofahamu kabla ya kikao hicho, naye aliingilia mlango wa nyuma.

Pamoja na wachezaji kutokea mlango huo, kimuonekano hawakuwa na nyuso za furaha, ingawa haikujulikana kabla kama ni uchovu ama wamefutwa kazi.

Lakini kwa upande wa wachezaji ambao walitokea mlango wa mbele ni David Molinga, Mrisho Ngassa, Metacha Mnata, Adeyun Seleh, Fei Toto.

Wengine ni Erick Kabamba, Farouk Shikalo, Ykpe na Juma Abdul, baadhi yao waliogopwa kusogelewa na mashabiki wao.