Nyota Simba, Yanga wafunguka Zahera kutemwa Yanga

Muktasari:

Yanga inahitaji ushindi wa mabao 2-0 au zaidi kwa Pyramids ili kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Dar es Salaam. Wakati hatma ya kocha Mwinyi Zahera ikiwa shakani nyota wa zamani wa Yanga na Simba wamemkingia kifua kocha huyo.

Zahera hivi karibuni alikutana na shubiri ya mashabiki kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza wengine wakimrushia chupa na wengine wakionyesha mabango ya kutaka afukuzwe.

Tukio hilo lilitokea baada ya Yanga kuruhusu kipigo cha mabao 2-1 nyumbani katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri matokeo yanayoweka shakani kibarua chake Yanga.

Pamoja na kwamba baadhi ya makocha wametajwa kumrithi Zahera Yanga, nyota wa zamani wa timu hiyo wamesema uamuzi wa Yanga kuachana na Zahera unapaswa uangaliwe kwa upana.

"Ni kweli mashabiki na wapenzi wa Yanga wana haki kwani furaha yao siku zote ni matokeo, wanapoona wamefungwa nyumbani lazima wasikitike," alisema nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella.

Alisema hata hivyo Yanga haipaswi kumuondoa kocha Zahera kwa mihemko ya mashabiki, lazima waangalie faida na athari watakapoachana naye.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema suala la mabadiliko ya benchi la ufundi sio mtizamo wa mtu mmoja na likifanyika lazima kuwe na sababu.

"Walinganishe msimu uliopita alichokifanya na msimu huu ambapo ni kweli Zahera amefanya usajili msimu huu kwa asilimia 95, hivyo kama uongozi ukiona kutakuwa na ulazima wa kumuondoa watafanya hivyo, lakini si kwa shinikizo.

Mshambuliaji nyota wa zamani wa timu hiyo, Peter Tino alisema Yanga isifanye uamuzi kwa presha ya mashabiki, ifikirie mara mbili kama kweli kuna haja ya kuachana na kocha Zahera.

Mshambuliaji huyo alisema hamaki ya wanachama imetokana na matokeo na Pyramids kwani mzigo wa Yanga katika mchezo huo umeongezeka mara dufu.

Ingawa makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredirick Mwakalebela amesisitiza kuwa Zahera hawezi kupimwa kwa matokeo ya mechi na Pyramids.

"Mashabiki wanasahau wao ndiyo walikuwa wakimfagilia kocha Zahera msimu uliopita alipokuwa akiipa timu matokeo, bado tunayo nafasi, tutulie tuisapoti timu katika mechi ya marudiano," alisema Mwakalebela.