Nyota Namungo kusubiri Simba tu

Muktasari:

Namungo ilitinga fainali ya michuano hiyo, baada ya kuifunga Sahare kwa bao 1-0 mchezo uliopigwa katika dimba la Mkwakwani.

Dar es Salaam. Baada ya kikosi cha Namungo kutinga fainali ya kombe la FA, kocha wa timu hiyo Hitimana Thiery amesema, atawapumzisha baadhi ya wachezaji wake kwenye michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Namungo ilitinga fainali ya michuano hiyo, baada ya kuifunga Sahare kwa bao 1-0 mchezo uliopigwa katika dimba la Mkwakwani, Tanga juzi.

Akizungumza jana Hitimana alisema, atalazimika kufanya hivyo, ili kuwapa nafasi wale ambao hawajapata nafasi mara nyingi na hao wengine wasubiri mchezo wa fainali ya FA.

Alisema ushindani ni mkubwa katika FA kutokana na kila timu kuhitaji nafasi ya uwakilishi kwenye michuano ya kimataifa mwakani na ndio sababu ya kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.

“Wachezaji wangu wamekuwa wakiumiaumia na huo mchezo utakuwa na ushindani sasa wakiumia wengine ambao nawategemea itaniathiri japokuwa kuumia nayo ni mipango ya Mungu, hivyo nafikiria kuwapumzisha wachache tu”

Namungo itacheza na Mbeya City Jumatano na Jumamosi na Prisons michezo ambayo Hitimana alisema hana cha kupoteza kutokana na nafasi ambayo timu yake ipo katika ligi ikiwa ya nne na kujinyakulia pointi 60.