Nyota Harambee pasua kichwa kwa kocha

Muktasari:

Leo usiku, Stars iliyojichimbia kambini huko Paris Ufaransa, itaingia dimbani kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Madagascar kisha wataelekea Madrid kuwavaa DR Congo (Juni 15), kabla ya kuelekea Cairo (Juni 19), kwa ajili ya michuano hiyo.

ZIMEBAKI wiki mbili tu kabla ya kushuhudia Fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON 2019, zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19, ila mpaka sasa nyota wa Harambee Stars, timu ya taifa ya Kenya wanampasua kichwa Kocha Mkiuu wake, Sebasrien Migne.
Kocha huyo Mfaransa mpaka sasa hajui amchukue nani na amuache nani yupi kwa ajili ya kikosi cha mwisho cha kwenda kukinukisha kwenye fainali hizo za 32 zinazofanyikia nchini Misri, ikishirikisha timu 24.
Kwa sasa kikosi hicho kilichoweka kambi ya siku 19 mjini Paris, Ufaransa, inaundwa na wachezaji 27 na michuano hiyo wanahitajika wachezaji 23, wakataosafiri kwenda Misri na Mfaransa huyo ameshindwa kufanya maamuzi, hii ikitokana na uwezo wa wachezaji alionao kambini.
Usiku wa leo, Stars  itaingia dimbani kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Madagascar kisha wataelekea Madrid kuwavaa DR Congo (Juni 15), kabla ya kuelekea Cairo (Juni 19), kwa ajili ya michuano hiyo.
Akitoa tathmini ya hali ilivyo kambini kabla ya kuwavaa Madagascar, Migne alisema mchezo wa leo wala haumnyimi usingizi ila uamuzi wa wachezaji atakaowanyoa na watakaobaki.
“Sio rahisi kuamua. Ugumu upo hapo tu, maana ukiangalia wachezaji wote wako fiti, lazima niwapunguze hadi 23, najua huu utakuwa mtihani, maana wakati mwingine mshikamano na umoja kikosini huathiriwa na uchaguzi," alisema Migne
NGOME IMARA
Aidha, Migne alisema kama alivyofanya katika mechi za kufuzu, atahakikisha ngome ya Stars inakuwa imara zaidi na hairuhusu mabao ya kizembe huku akisisitiza kuwa hiyo ndio njia pekee ya kuwazuia Mbwana Samatta, Sadio Mane na Riyadh Mahrez.
"Katika hatua ya kufuzu tulifanikiwa katika hilo, tiliweza kuwazuia Ghana. Lengo letu ni kufuzu hatua inayofuata, silaha yetu ni kuwazuia akina Samatta, Mane na Mahrez, kila anajua ninachozungumzia," alisema.
Kenya, ambayo ipo kundi C pamoja na Tanzania, Senegal na Algeria, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal, Julai mosi. Mechi zote zitapigwa Cairo, katika uwanja wa June 30.
KIKOSI KILICHOKO KAMBINI
Makipa: Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo
Mabeki: Abud Omar, Joash Onyango, Joseph Okumu, Musa Mohammed, David Owino, Bernard Ochieng, Brian Mandela, Philemon Otieno, Eric Ouma
Viungo: Victor Wanyama, Anthony Akumu, Ismael Gonzalez, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ovella Ochieng, Dennis Odhiambo, Eric Johanna, Paul Were, Cliffton Miheso, Johanna Omollo
Mastraika: John Avire, Masud Juma, Christopher Mbamba, Michael Olunga