Nyota 6 Simba wa kupindua meza

Muktasari:

Kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kuzuia na kuchezesha timu, Sharaf Shiboub aliyenaswa na Simba kutokea Sudan, anaweza kuwa mmoja wa nyota muhimu watakaoifanya timu hiyo iendelee kung’ara msimu ujao.

SIMBA imefanya usajili wa nguvu kwa kujaza kundi kubwa la mastaa ambao litawapa wigo mpana kwa benchi lao la ufundi katika uteuzi wa wachezaji wa kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, katika kundi hilo la wachezaji waliosajiliwa na Simba, ubora na ufanisi wa mastaa sita huenda ukawa chachu kwa timu hiyo kutamba kwa mara nyingine kwenye mashindano mbalimbali itakayoshiriki kama ilivyofanya msimu uliopita.

Nyota hao sita ni kipa Beno Kakolanya, beki Shomary Kapombe, kiungo Sharaf Shiboub na washambuliaji Ibrahim Ajibu, Deo Kanda na Meddie Kagere.

Pamoja na uwezo mkubwa wa wachezaji waliosajiliwa na Simba, wakali hao sita wanaonyesha ishara ya wazi kuwa wataibeba timu hiyo ikiwa wataweza kulinda makali na ubora wao.

Uwepo wa kipa Beno Kakolanya, unaipa Simba uhakika wa uimara kwenye lango lake kutokana na uwezo mkubwa wa nyota huyo wa zamani wa Yanga, Prisons na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuondoa hatari langoni mwake hasa yale mashambulizi ya ana kwa ana.

Pia kipa huyo ataisaidia Simba kwa kumpa changamoto Aishi Manula ambaye ni wazi ataimarika kiwango ili kukwepa mtego wa kusotea benchi.

Mchezaji mwingine ni Kapombe ambaye kurejea kwake ndani ya kikosi cha Simba ni kama usajili mpya kutokana na ubora na mchango wake.

Uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi mbili uwanjani, kasi, stamina na namna anavyoweza kuhusika katika kutengeneza mashambulizi vitakuwa chachu kwa Simba kufanya vizuri, lakini hilo litafanikiwa kwa kiasi kikubwa ikiwa hatapata majeraha ambayo yamekuwa yakimsumbua mara kwa mara.

Kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kuzuia na kuchezesha timu, Sharaf Shiboub aliyenaswa na Simba kutokea Sudan, anaweza kuwa mmoja wa nyota muhimu watakaoifanya timu hiyo iendelee kung’ara msimu ujao.

Shiboub tayari ameshaanza kuteka hisia za mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kutokana na kiwango bora alichoonyesha kwenye mechi alizoichezea na ameonekana kumudu upesi staili ya timu hiyo.

Pamoja na kucheza kama kiungo wa ulinzi, Shiboub ana uwezo pia wa kufunga jambo ambalo litazidi kuiongezea makali Simba kwenye kufumania nyavu.

Nyota wengine ambao ni wazi watakuwa na mchango mkubwa kwa Simba ni Ibrahim Ajibu na Deo Kanda.

Ajibu ana uwezo wa hali ya juu wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao na ni wazi kwamba ubunifu wake utaisaidia safu ya ushambuliaji ya Simba na hilo ndilo linaonekana kwa Kanda ambaye uzoefu na uwezo wake wa kucheza kama winga wa pembeni utakuwa chachu ya kuzalisha mabao.

Lakini, kasi ya kupachika mabao ya mshambuliaji Meddie Kagere inaendelea kuwapa tumaini Simba katika msimu ulioanza wakimtegemea aendelee kuwa mkombozi wao kwa mara nyingine.

Msimu uliopita, Kagere aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu na mabao yake 23 lakini pia alishika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao sita.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kuwa usajili wa timu hiyo ni mzuri na utaisaidia kwa vile umezingatia mahitaji ya benchi la ufundi.

“Wachezaji sio wabaya na kila nafasi ukitazama ina wachezaji kama sio wawili basi watatu wa nafasi moja jambo linaloongeza ushindani wa namba kikosini.

Nadhani kama timu ikikaa sawa na wakapata muunganiko mzuri basi Simba itafanya vizuri zaidi,” alisema Pawasa.

Mchambuzi wa soka, Mwalimu Alex Kashasha alisema ubora wa mchezaji husika katika kumudu majukumu ya kitimu ndio utakaoipa mafanikio Simba.

“Kuna vitu vya msingi ambavyo timu huzingatia wakati wa kufanya usajili. Kuna wachezaji ambao wanaitwa versatile (wenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani), hawa ndio wana nafasi kubwa ya kupata nafasi ya kucheza,” alisema Kashasha.

“Simba wana kikosi kizuri na wachezaji wake wengi wana uwezo mkubwa hivyo wataisaidia kwenye mashindano ambayo yako mbele yao.”