Nyota 15 Yanga waendelea na mazoezi

YANGA imeendelea na mazoezi ikiwa ni siku ya pili tangu itangaze kuanza kambi huku wachezaji 15, wapya watatu na 12 wa zamani walikuwa wakijifua katika Uwanja wa Chuo cha Sheria Simu 2000, kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Mazoezi hayo yanafanywa chini ya kocha wa Yanga B, Said Maulidi 'SMG' na miongoni mwa nyota waliokuwa nao tangu msimu ulioisha ni kipa Metacha Mnata, Ramadhani Kabwili, mabeki Adeyum Saleh, Paul Godfrey na Said Makapu.

Wakati viungo ni Feisal Salum 'Fei Toto', Abdulaziz Makame na Deus Kaseke, washambuliaji ni Adam Kiondo wa timu B, Juma Mahadhi na Ditram Nchimbi.

Wapya ambao Yanga imewasajili na wameungana na wenzao katika mazoezi hayo ni beki Yassin Mustapha (Polisi Tanzania), straika Wazir Junior (Mbao FC) na kiungo Zawadi Mauya (Kagera Sugar).

MAZOEZI YALIVYOKUWA

Kaseke bado anaonekana yupo fiti katika mazoezi hayo, alikuwa mwepesi wakupiga mipira, kasi na pumzi.

Wakati huo huo kiungo Feisal Salum naye alikuwa yupo vizuri wakifanya mazoezi mbalimbali.

Kwa upande wa wapya ambao ni Mustapha, Junior na Mauya pia walionyesha bidii, wakionekana wanapumzi yakutosha.

SMG alianza kwa kuwataka wachezaji wake waanze kukimbia na baada ya dakika 15 alibadili mazoezi na kuwataka wachezaji wakimbie na mipira kila mmoja.

Zoezi hilo kila mchezaji alitakiwa kuongeza umakini kwa kuweka utulivu kwenye mguu wake akiwa na mpira mguuni, kabla ya kupiga pasi.

Baada ya zoezi hilo, SMG alikuwa anawapanga wachezaji katika kona mbili na alikuwa anawataka wakimbie spidi kwa kupishana kwa kona.