Nyoni amvuruga Aussems Simba

Muktasari:

  • Jana Jumatatu asubuhi, Nyoni alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kipimo kikubwa cha MRI ambapo ilibainika tatizo lake litamweka nje kwa wiki hizo japo viongozi wake waliendelea kuhaha kuhakikisha anapatiwa matibabu ya haraka ili asikae nje kwa kipindi kirefu.

KUUMIA kwa beki Erasto Nyoni, kumemchanganya Kocha wa Simba, Patrick Aussems kwani muda atakaokaa nje kwa wiki tatu kunamfanya kocha huyo kukipangua kikosi chake.

Nyoni aliumia kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM juzi Jumapili usiku kiasi cha kushindwa kuendelea na pambano hilio. Kitendo hicho kimemfanya Aussems kupangua kikosi chake ambapo sasa anatarajia kumtumia, Juuko Murshid ambaye hapewi nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Viongozi wa Simba wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Crescentius Magori ambao walishuhudia mechi hiyo ya KMKM, walimuwahisha mchezaji wao hospitali ambako alipatiwa matababu ya awali na kufanya kipimo cha x-ray.

Jana Jumatatu asubuhi, Nyoni alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kipimo kikubwa cha MRI ambapo ilibainika tatizo lake litamweka nje kwa wiki hizo japo viongozi wake waliendelea kuhaha kuhakikisha anapatiwa matibabu ya haraka ili asikae nje kwa kipindi kirefu. Njia pekee ya kujiridhisha ni pale ambapo viongozi wa Simba waliamua kumrudisha Nyoni jijini Dar es Salaam mchana wa jana Jumatatu kwa ajili ya vipimo zaidi.

Juuko anatarajiwa kucheza pambano hilo ikiwa ni kipimo chake kuelekea mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya JS Saoura ya Algeria itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

“Juuko ni mchezaji mzuri ila anapaswa kupambana kuitetea timu yake, ambapo kesho (leo Jumanne) itabidi acheze mechi yetu nyingine ambayo tutacheza kabla ya kurudi Dar es Salaam kupambana na wapinzani wetu kimataifa. alisema Aussems.

Kagere, Mkude watengewa mazoezi

Jonas Mkude na Meddie Kagere katika mazoezi ya jana Jumatatu asubuhi usiku walitengewa mazoezi maalumu kutokana na sababu tofauti.Mkude yeye alijiunga na kikosi hicho juzi wakati Kagere yeye ilidaiwa kuwa alipatwa na majeraha ambapo wawili hao walisimamiwa na kocha wa viungo Zrane Adel.

Aussems jana aliamua kuwapa mapumziko nyota wake wawili washambuliaji John Bocco na Emmanuel Okwi ambao hawakufanya mazoezi kabisa na wenzao. “Hawaumwi nimeamua tu wapumzike maana huu uwanja sio mzuri kwa mchezaji,”.

Mabosi presha tupu

Viongozi wa Simba waliowasili Kisiwani hapa kushuhudia mechi za Mapinduzi za timu yao wameonekana kuwa na presha kubwa baada ya Nyoni kuumia.