Nyoni, Yondani, Bocco usipime Taifa Stars

Muktasari:

Ushindi huo unaifanya Tanzania kuwa katika nafasi ya pili katika Kundi L na kufufua matumaini yake ya kusaka kufuzu kwa AFCON2019, Cameroon

Dar es Salaam. Wachezaji Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na mshambuliaji John Bocco wamethibisha ubora wao kwa kuiongoza Taifa Stars kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde.

Katika mchezo huo mabao ya Taifa Stars yalifungwa na Simon Msuva na Mbwana Samatta huku wakongwe Nyoni na Yondani na Bocco aliyeingia kipindi cha pili wakionyesha soka la kiwango cha juu.

Nyoni na Yondani katika mchezo uliopita nchini Cape Verde hawakupata nafasi ya kucheza, huku Bocco akiingia katika dakika kumi za mwisho.

Kwa upande wa Nyoni yeye alikuwa hajaitwa katika kikosi cha Stars, lakini baada ya kurejea ameonyesha alistahili kurejeshwa kwani aliitendea kazi nafasi ya kiungo mkabaji kuziba vizuri pengo la Frank Domayo.

Bocco naye licha ya kuchezeshwa kama winga, alikuwa akicheza kwa kujituma na kasi yake kukomaa kwa kushambulia na kukaba kadri dakika zilivyokiwa zinazidi kwenda.

Katika safu ya ulinzi Aggrey na Yondan walionyesha ukubwa wao kwani walikuwa hawana masihara kwa mpira wowote uliokuwa unapita ndani ya kumi nane.

Ushindi wa Stars katika mchezo huu ulitokana na mbinu za kocha Emmanuel Amunike alikuwa akitumia tofauti na mechi iliyopita.

Katika mchezo huu Stars walikuwa wakitumia mipira mirefu kupeleka mashambulizi, mbinu hii ilikuwa ikiwasumbua Cape Verde katika kuzuia.

Kasi ya Msuva, Kapombe na Gadiel Michael katika kupeleka mashambulizi ulikuwa mwiba kwa kikosi cha Cape Verde.

Mabadiliko ya safu ya kiungo yalikuwa na tija katika mchezk huu kwasababu maelewano ya Nyoni, Mao na Mudathir katika kipindi cha kwanza yaliifanya Stars wacheze soka la kuvutia.

Hata walipofanya mabadiliko kwa kumtoa Mudathir na kumuingiza Feisal Salum bado safu hiyo katika kiungo ilizidi kuwa imara.