Nyoni: Bado Moja

Muktasari:

Licha ya Simba kulitwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara mara ya tatu mfululizo msimu huu, bado malengo yao hayajatimia kwani nia yao kubwa ni kulitwaa na kombe la FA ambapo watakutana na Namungo iliyopanda ligi msimu huu.

BEKI kisiki wa klabu ya Simba, Erasto Nyoni amesema, licha ya kuwafunga Yanga katika mchezo wa jana, bado wanahitaji kuifunga Namungo katika mchezo wa fainali Agosti 2 mwaka huu ili watimize malengo yao.

Nyoni moja ya mabeki bora kwa sasa, amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Wanamsimbazi kutokana na umahiri wake wa kumlinda mlinda mlango wake asitikiswe mara kwa mara na wapinzani.

Nyoni ameyasema hayo jana kuwa, mpaka sasa wametimiza lengo moja la ubingwa wa Ligi Kuu bado kombe la FA kwa kuwa nalo liko katika mipango yao ya msimu huu.

Amesema, ya jana kuwafunga Yanga mabao 4-1 yameisha na wanamshukuru Mungu kwa matokeo hayo.

"Ubingwa wa ligi tayari, hilo lilikuwa lengo namba moja, namba mbili ni kombe la FA ambalo nalo kwa uwezo wa Mungu tutalitwaa tu,"

"Kikubwa zaidi sisi wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki tuendelee kuwa kitu kimoja kuhakikisha tunamfunga Namungo naimani tutaweza na kufanikisha,"

Aidha Nyoni aliwapongeza wachezaji wenzaake kwa umoja wa hali ya juu ambao wako nao na ndiyo sababu kubwa ya kutimiza malengo yao ndani ya mwaka huu kwani wembe ndio ule ule uliowanyoa Azam umewanyoa Yanga na sasa Namungo ajiandae.

Kwa sasa wachezaji wote wa Simba wamepewa mapumziko wa siku mbili leo na kesho kabla ya kurejea kuendelea na kujiandaa na mechi dhidi ya Mbao Alhamisi.