Nyirenda amzuia Banda

Muktasari:

  • Kocha huyo, alisema Baroka ya msimu ujao wa 2019/20 itakuwa tofauti na msimu uliopita kutokana na namna ambavyo anataka kukisuka upya kikosi hicho.

BAADA ya Baroka FC, anayoichezea beki Mtanzania, Abdi Banda kunusurika kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’, kocha wa timu hiyo, Wedson Nyirenda amesema anataka kukisuka upya kikosi chake.

Nyirenda kwenye moja ya mahojiano yake, baada ya msimu huu wa 2018/19 kumalizika, alisema jukumu alilopewa kipindi alipopata kibarua cha kuinoa klabu hiyo ilikuwa ni kuinusuru isishuke daraja.

Kocha huyo, alisema Baroka ya msimu ujao wa 2019/20 itakuwa tofauti na msimu uliopita kutokana na namna ambavyo anataka kukisuka upya kikosi hicho.

“Kuna wachezaji wapya ambao tutawaongeza kwenye baadhi ya maeneo, lengo ni kutaka tuwe na kikosi kipana, nina matumaini wachezaji wangu muhimu watasalia.

“Kumekuwa na tetesi nyingi lakini nitafanya kitakachokuwa ndani ya uwezo wangu. Majeraha ya baadhi ya wachezaji ni kitu ambacho kilituyumbisha kipindi fulani,” alisema kocha huyo. Kilichoibeba Baroka kusalia Ligi Kuu Afrika Kusini ni sare ya bao 1-1 dhidi ya Maritzburg United.

BANDA YUPO YUPO

Nyirenda anataka kubaki na wachezaji wake muhimu na huenda Abdi Banda akasilia kwenye klabu hiyo. Dalili zimeanza kuonekana kwa Banda kubaki kwenye klabu hiyo, baada ya kuandika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa ataonana na mashabiki wa timu hiyo msimu ujao.

“Nina furaha kuumaliza msimu salama, nashukuru kwa sapoti ya kila mmoja, tukutane tena msimu ujao,” aliandika Banda.